ILO: Upatikanaji wa kazi zenye ubora wadorora duniani, vijana na wanawake wakiumia zaidiILO: Upatikanaji wa kazi zenye ubora wadorora duniani, vijana na wanawake wakiumia zaidi

Hayo ni kwa mujibu wa ripoti mpya ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kazi duniani (ILO) iitwayo Hali ya Ajira na Mitindo ya Kijamii Duniani 2026 (WESP 2026) iliyotolewa leo jijini Geneva, Uswisi. Ripoti hiyo inaonya kuwa vijana wanaendelea kuhangaika kupata ajira, huku akili mnemba (AI) na kutokuwepo kwa uhakika wa sera za biashara kukihatarisha soko la ajira.

media:entermedia_image:7a2e41bd-0945-4190-8950-37d50afec316

© ILO/Marcel Crozet

Wanawake wanafanya kazi katika kiwanda cha kutengeneza viatu nchini Kambodia.

Ripoti imegundua kuwa wakati kiwango cha ukosefu wa ajira duniani kinakadiriwa kusalia kwa asilimia 4.9 mwaka 2026 sawa na watu milioni 186, mamilioni ya wafanyakazi duniani kote bado hawana upatikanaji wa kazi bora.

Mkurugenzi Mkuu wa ILO, Gilbert F. Houngbo, akizungumzia ripoti hiyo amesema, “ukuaji thabiti na takwimu thabiti za ukosefu wa ajira hazipaswi kutuvuruga kutoka kwenye ukweli wa kina: mamia ya mamilioni ya wafanyakazi wamekwama katika umaskini, ukosefu wa mifumo rasmi, na kutengwa”

Ripoti inabainisha kuwa karibu wafanyakazi milioni 300 wanaishi katika umaskini uliokithiri, wakipata chini ya dola 3 za Marekani kwa siku. Aidha, idadi ya wafanyakazi katika sekta isiyo rasmi inatarajiwa kufikia bilioni 2.1 ifikapo mwaka 2026, wakiwa hawana ulinzi wa kijamii wala usalama wa kazi.

media:entermedia_image:c54b0aca-5b61-4351-b0f4-c5b04161b7b3

UN News/Conor Lennon

Roboti yenye uwezo wa kutumia AI ikitembea kwenye korido za Mkutano wa ngazi za juu wa Sekta ya Kimataifa wa UNIDO wa 2025 huko Riyadh, Saudi Arabia.

Changamoto kwa vijana na Akili Mnemba (AI)

Ukosefu wa ajira kwa vijana ulipanda hadi asilimia 12.4 mwaka 2025. Takriban vijana milioni 260 hawako shuleni, hawana ajira, wala hawako kwenye mafunzo yoyote ya ujuzi. ILO imeonya kuwa matumizi ya akili mnemba (AI) na mitambo ya kujiendesha yanaweza kuongeza ugumu wa kupata kazi, hasa kwa vijana wasomi katika nchi tajiri wanaotafuta kazi za ujuzi wa juu kwa mara ya kwanza.

Ubaguzi wa kijinsia na mabadiliko ya idadi ya watu

Wanawake bado wanakabiliwa na vikwazo vikubwa kutokana na mila na mitazamo potofu. Wanachangia asilimia 40 tu ya ajira duniani, na wana uwezekano mdogo wa asilimia 24 kushiriki katika soko la ajira ikilinganishwa na wanaume.

Vilevile, ripoti inabainisha kuwa kuongezeka kwa idadi ya watu wenye umri mkubwa katika nchi tajiri kunapunguza nguvu kazi, huku nchi maskini zikishindwa kugeuza ongezeko la watu kuwa fursa za ajira zenye tija.

Mabadiliko ya idadi ya watu na biashara duniani

Ripoti ya ILO inabainisha kuwa mabadiliko ya idadi ya watu yanapanga upya masoko ya ajira; nchi tajiri zinakabiliwa na uhaba wa nguvu kazi kutokana na kuongezeka kwa wazee, wakati nchi maskini zinahangaika kugeuza ongezeko kubwa la vijana kuwa ajira zenye tija. Bila nafasi za kazi, nchi maskini zinahatarisha kupoteza faida ya nguvu kazi ya vijana.

Mwanabiashara anatembea kwenye soko katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.

© IMF/Stephen Jaffe

Mwanabiashara anatembea kwenye soko katika Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Wakati huo huo, misukosuko ya kibiashara duniani inasababisha hali ya kutojua hatma ya ajira na kupunguza mishahara, hasa barani Asia na Ulaya. Pamoja na hayo, biashara inasalia kuwa chanzo kikuu cha ajira kwa watu milioni 465 duniani, ikitoa fursa bora kwa wanawake na vijana. Mkurugenzi Mkuu wa ILO amesisitiza uhitaji wa hatua za pamoja ili kuhakikisha nchi maskini hazichiwi nyuma na upanuzi wa biashara ya kidijitali na minyororo ya ugavi.

“Isipokuwa serikali, waajiri, na wafanyakazi washirikiane kutumia teknolojia kwa uwajibikaji na kupanua fursa za kazi bora kwa wanawake na vijana, uhaba wa kazi zenye staha utaendelea na mshikamano wa kijamii utakuwa hatarini.” – Gilbert F. Houngbo, Mkurugenzi Mkuu wa ILO.

Wito wa hatua za pamoja

Mkurugenzi Mkuu Houngbo ametoa wito kwa serikali, waajiri, na wafanyakazi kushirikiana kuwekeza katika ujuzi, miundombinu, na kutumia teknolojia kwa kuwajibika ili kuziba pengo la usawa na kukuza haki za kijamii.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *