Mama Diamond amjibu mke wa Fella, akumbushia Sh5 milioniMama Diamond amjibu mke wa Fella, akumbushia Sh5 milioni

Dar es Salaam. Ikiwa imepita wiki moja tangu Sweet Fella ambaye ni mke wa aliyekuwa meneja wa wasanii wa muziki Bongo Said Fella ‘Mkubwa Fella’ kulalamika kukosa ushirikiano wa kimatibabu kutoka kwa watu wa karibu wa mumewe. Hatimaye mama wa mwanamuziki Diamond ametoa neno.

Katika  mahojiano aliyofanya mke wa Fella na Mwananchi baada ya kuachia ujumbe wa kutopendezwa na walioingia mitini baada ya Fella kuugua, alisema Diamond aliwasaidia kumpeleka mgonjwa India kwa mara ya kwanza lakini baada ya hapo alikaa kimya.

“Kuhusu Diamond Platnumz, kutomsaidia Fella, yaani huwezi kumlazimisha mtu kwamba kwanini husaidii? Kwani yeye mwenyewe hajui kama Fella anaumwa? Si anajua bosi wake anaumwa.

“Hata kama ndio alitusaidia tukaenda India tukarudi, lakini asingeishia njiani na kukaa kimya. Sasa mimi kama nimetoa dukuduku langu sisaidiwi na mtu maana watu wanaweza kusema napata msaada kwa Diamond ambaye ni tajiri anamsaidia,”alisema

Hata hivyo, baada ya hayo mama mzazi wa Diamond, Sanura Kassim a.k.a Mama Dangote kupitia ukurasa wake wa Instagram amemtaka mke wa Fella kuwa na shukrani.

“Mungu atakulipia kwa kila ulichokifanya!. Lakini pia akumbuke Mrs Fellah wa kwanza kunipigia simu ni mimi, Simba alikuwa hayupo nchini nami nikaenda mpaka Mbagala sijui kunaitwa Kilungule Hospital alipolazwa.

“Nilipompigia simu Simba aliniuliza mama hujatoka na pesa hapo, mwambie Makame amtumie mke wa Fella milioni tano hiyo ndio siku ya kwanza kabla ya kumpeleka TMJ HOSPITAL na INDIA jamani binadamu tushukuru mtoto wa mtu akijitoa kwenye jambo la mtu tuwe na shkurani,”ameandika Mama Dangote

Ikumbukwe Machi, 4, 2025 Mwananchi iliripoti hali ya kiafya ya Mkubwa Fella aliyekuwa akisumbuliwa na presha na kupooza miguu. Hata hivyo  Fella alisema afya yake imezidi kuimarika baada ya kutoka India kupata matibabu, ambapo huko India gharama zote aligharamia Diamond Platnumz .

Ilipofika Mei, 2025  Fella alisema kutokana na hali yake kuwa mbaya kwa matatizo hayo. Alikata tamaa ya kupona lakini kwa wakati huo anamshukuru Mwenyezi Mungu kwani anaendelea vizuri.

“Nina furaha kwani kwa sasa naendelea vizuri, hali yangu inaimarika kila siku na nimeanza kufanya mazoezi ya kutembea kila ifikapo jioni.

“Ukweli mimi nimeumwa sana yaani nimeumwa kweli hadi nikawa nimekata tamaa ya kupona, ila namshukuru Mungu sana hadi sasa naweza kuongea na wewe hivi na kutembea vizuri kwa kufanya mzoezi, ilikuwa balaa,” amesema Mkubwa Fella.

Taarifa za kuumwa kwa Said Fella ‘Mkubwa Fella’ ziliibuka kwenye mitandao ya kijamii Januari , 2025 kuwa amepoza miguu huku wengi wakidai Diamond amemtelekeza.

Hata hivyo baada ya kupata taarifa hizo Mwananchi ilimtafuata nyumbani kwake Mbagala kata ya Kilungule, jijini Dar es Salaam na kuzungumza na baadhi ya ndugu zake ambao walidai hali yake haikuwa nzuri hata kuzungumza na mtu kwa muda mrefu alikuwa anashindwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *