Mswada wa kuifanya Greenland jimbo la Marekani wawasilishwaMswada wa kuifanya Greenland jimbo la Marekani wawasilishwa

Mbunge wa Republican kutoka Florida amewasilisha mswada unaopendekeza kuiunganisha Greenland na kuifanya kuwa jimbo la 51 la Marekani, wakati Rais Donald Trump akiendelea kutishia kulinyakua eneo hilo linalojiendesha chini ya utawala wa kifalme wa Denmark.

Mbunge huyo, Randy Fine, amesema mswada huo ungempa Trump mamlaka ya “kuchukua hatua zozote zinazohitajika” kuiunganisha Greenland na kuifanya sehemu ya Marekani.

Trump amewahi kusema kwamba Marekani itaichukua Greenland “kwa njia moja au nyingine” akitaja uwezekano wa kununua eneo hilo au kulichukua kwa nguvu, licha ya upinzani mkali kutoka Denmark, ambayo ni mshirika wa muungano wa kujihami wa NATO.

Ameeleza kuwa Greenland, yenye utajiri mkubwa wa madini adimu, ni muhimu kwa usalama wa taifa la Marekani na inapaswa kuwa chini ya udhibiti wake.

Hata hivyo kauli zake zimepingwa na wabunge wa vyama vyote viwili, huku Waziri Mkuu wa Denmark, Mette Frederiksen, akionya kwamba shambulio lolote la kijeshi la Marekani dhidi ya Greenland lingeuweka hatarini muungano wa NATO.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *