
Tangu Urusi ilipoanzisha uvamizi kamili dhidi ya jirani yake mwezi Februari 2022, Umoja wa Mataifa na washirika wake wamekuwa wakisaidia watu wenye uhitaji kwa kushirikiana na juhudi za Serikali, kuanzia wakazi wa mijini wanaoendelea kukabiliwa na mashambulizi ya mara kwa mara ya ndege zisizo na rubani au droni na makombora, hadi jamii zilizo karibu na mstari wa mbele wa mapigano na wengine waliokimbizwa mbali na maeneo ya hatari.
“Ninazungumzia wakimbizi wa ndani watu waliokimbia makazi yao ambao wamekuwa katika maeneo ya makazi ya pamoja kwa miaka miwili au mitatu, ninazungumzia wazee na watu wenye uhamaji mdogo,” amesema Matthias Schmale, afisa mkuu wa misaada wa Umoja wa Mataifa nchini Ukraine, akieleza baadhi ya vipaumbele vya ombi la misaada lililozinduliwa Jumanne.
Mashambulizi zaidi ya 1000 kwa wiki moja
Kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari na taarifa rasmi kutoka kwa mamlaka za Ukraine, katika kipindi cha wiki moja pekee iliyopita, majeshi ya Urusi yalirusha karibu droni 1,100 za kushambulia Ukraine, zaidi ya mabomu ya angani 890 na angalau makombora 50 ya aina mbalimbali yakiwemo makombora ya balistiki na ya kuruka chini pamoja na kombora la masafa ya kati la balistiki aina ya Oreshnik lililolenga mji wa Lviv magharibi mwa Ukraine, karibu na mpaka wa Poland.
Mbali na kutoa msaada wa msingi wa kibinadamu, ikiwa ni pamoja na chakula, huduma za afya, makazi, ulinzi na msaada wa fedha taslimu, malengo mengine muhimu ya ombi la ufadhili la Jumanne ni kusaidia kuwaondoa watu walio katika hatari ya haraka “kazi za kishujaa karibu na mstari wa mbele,” amesema Bwana. Schmale, akirejelea mamia ya washirika wanaoungwa mkono na Umoja wa Mataifa wanaotekeleza kazi hii ya kuokoa maisha.
Mahitaji katika mstari wa mbele
Ameeleza kuwa ufadhili unahitajika kusaidia washirika wa asasi za kiraia wanakabili mashambulizi ya kijeshi kote nchini lakini hasa ndani ya kilomita 50 kutoka mstari wa mbele wakisaidia wakulima wanaojaribu kuishi katika maeneo ya vita, pamoja na wagonjwa wa saratani ambao upatikanaji wao wa dawa umevurugika kutokana na mashambulizi yanayoathiri huduma za afya.
“Tunataka kuendelea kusaidia kwa kadri tuwezavyo, lakini yote haya yanahitaji ufadhili,” amesema Bwana. Schmale.
Alisisitiza “mateso makubwa ya raia kote Ukraine, hasa wakati jamii zinapokabiliwa na kushuka kwa kiwango cha joto hadi nyuzi joto -15°C mjini Kyiv ni dharura ndani ya dharura” ambayo huenda ikahitaji ufadhili zaidi kutoka kwa jumuiya ya kimataifa, juu ya ombi la leo, amebainisha Mratibu wa Masuala ya Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa.
“Tunaomba hasa jumuiya ya kimataifa, Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa, na wafadhili wengine, kuendelea kudumisha mshikamano wao na Ukraine na kuonesha hilo kwa msaada wa kifedha kwa kazi tunazopanga kuendelea nazo,” amesema.
Akizungumza mjini Kyiv wakati wa uzinduzi wa ombi hilo, Bw. Schmale ameelezea pia taarifa mpya kutoka kwa timu ya Umoja wa Mataifa ya ufuatiliaji wa haki za binadamu, ikionesha kuwa mwaka 2025 ulikuwa mwaka mbaya zaidi kwa raia tangu 2022, huku zaidi ya raia 2,500 wakiuawa na zaidi ya 12,000 kujeruhiwa.
