
Maandamano yaliyoikumba Iran yamechochewa na mbinyo mkubwa wa kiuchumi; na kutokana na Wairani kuona jinai zilizofanywa na Israel na kile ambacho Marekani imekifanya nchini Venezuela, madai hasa ya wananchi hao si kutaka ufanyike uingiliaji wa kijeshi wa madola wageni dhidi ya nchi yao. Hayo yameelezwa na wataalamu kadhaa wa kikanda.
Wakizungumza katika hafla iliyoandaliwa na Taasisi ya Quincy for Responsible Statecraft jana Jumatatu, wataalamu hao wamesema, japokuwa kunaweza kukawepo na sauti ambazo ni za nje, Wairani wengi wanataka jamii ya kimataifa isaidie kuondolewa vikwazo vinavyolemaza vya Marekani na kuanza njia mpya kwa nchi yao kusonga mbele.
“Nadhani [idadi kubwa] ya Wairani wangekaribisha makubaliano ambayo yanaondoa kivuli cha vita na kutoa mwito wa kuondolewa vikwazo,” amesema Mohammad Ali Shabani, mhariri wa jarida la habari la Amwaj.
Naye, Ellie Geranmayeh, mshiriki mwandamizi wa sera na naibu mkuu wa mpango wa Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini katika Baraza la Ulaya la Mahusiano ya Kigeni, yeye ametilia mkazo na kuunga mkono hoja hiyo na kusema: “nadhani mara nyingi sisi Magharibi, tunasahau kwamba [jamii ya kiraia ya Irani] ipo, na kwamba watu hao hawajawa wakitaka kuwepo uingiliaji wa maajinabi kupitia mashambuulio ya kijeshi, na hawajawa wakitaka maandamano kugeuzwa kuwa ya vurugu”…/