Seneta wa Marekani Mark Warner amesema, nchi hiyo inakabiliwa na ongezeko la ubaguzi wa kidini na misimamo ya kufurutu mpaka inayochochewa na chuki, akiishutumu serikali ya Trump kwa kuchangia kuongezeka kwa hisia za uenezaji hofu na chuki dhidi ya Uislamu (Islamophobia) na hisia za kupiga vita Waarabu.

“Ninasimama leo kulaani, hasahasa ubaguzi zinaofanyiwa jamii zetu za Waislamu na Waarabu wa Marekani, kwa sababu, kwa masikitiko, rais huyu na serikali yake wamejitokeza hadharani kuchochea na kurasimisha ubaguzi wa chuki dhidi ya Uislamu” ameeleza Warner.

Kwa kutoa mfano, Seneta huyo wa Marekani ameashiria matamshi aliyotoa Trump katika mkutano wa baraza la mawaziri mwezi uliopita kuhusu watu wenye asili ya Somalia, akisema rais huyo wa Marekani aliitaja jamii hiyo kama “takataka” na akasema, “hatuwataki wao katika nchi yetu.”

Warner ameyaelezea matamshi hayo ya Trump kuwa ni ya “kuchukiza, ya kudhalilisha utu, na yasiyo ya Kimarekani,” akisisitiza kwamba, yanapasa “kulaaniwa kwa sauti kubwa” na maafisa wote wa umma.

Seneta huyo amekosoa pia matamshi ya kichochezi yanayotolewa hata ndani ya Bunge la Marekani la Congres na kubainisha kuwa, seneta mwenzake ambaye hakumtaja jina, hivi karibuni aliuelezea Uislamu kama “dini yenye sumu” ambayo “kimsingi haiendani na maadili yao ya Magharibi.”

“Lakini sisi sote, hasa wale wanaohudumu katika chombo hiki katika ofisi za umma, tuna wajibu wa kukomesha ukimya huo na kulaani kwa sauti kubwa na kwa uthabiti chuki dhidi ya Uislamu na chuki dhidi ya Waarabu,” amesisitiza Warner…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *