WHO yaonya kuwa vinywaji vya bei rahisi vinaongeza magonjwa yanayozuilikaWHO yaonya kuwa vinywaji vya bei rahisi vinaongeza magonjwa yanayozuilika

Katika ripoti mbili mpya za kimataifa, WHO imesema ushuru mdogo na usiopangwa ipasavyo unaacha bidhaa zinazodhuru afya ziendelee kuwa rahisi kununua, wakati nchi nyingi zikikabiliwa na mifumo ya afya iliyoelemewa na mzigo wa magonjwa yasiyoambukiza NCDs na majeraha yanayozuilika.

“Kodi ya afya ni miongoni mwa nyenzo zenye nguvu zaidi tulizo nazo za kulinda afya na kuzuia magonjwa,” amesema Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus, Mkurugenzi Mkuu wa WHO. 

Ameongeza kuwa “Kwa kuongeza kodi kwenye bidhaa kama tumbaku, vinywaji vyenye sukari na pombe, serikali zinaweza kupunguza matumizi hatarishi na kufungua rasilimali za kifedha kwa huduma muhimu za afya.”

Utafiti mpya wahusisha unywaji wa pombe na kuongezeka kwa hatari ya saratani , ajali za barabarani na vifo

Brazil Agency Archive

Utafiti wahusisha unywaji wa pombe na kuongezeka kwa hatari ya saratani , ajali za barabarani na vifo

Bidhaa hatarishi ni nafuu, gharama za afya zinaongezeka

Katika ripoti hizo WHO imebainisha kuwa soko la kimataifa la vinywaji vyenye sukari na vileo huzalisha faida ya mabilioni ya dola kila mwaka. 

Hata hivyo, serikali hunufaika kwa kiwango kidogo tu kupitia kodi unaolenga afya, huku jamii zikibeba gharama za muda mrefu za kiafya na kiuchumi.

Kwa mujibu wa shirika hilo, mifumo dhaifu ya ushuru imeshindwa kuendana na mfumuko wa bei na ongezeko la kipato, jambo linalofanya pombe na vinywaji vyenye sukari kuwa nafuu zaidi kadri muda unavyopita katika nchi nyingi mwelekeo unaohusishwa moja kwa moja na matumizi makubwa na mzigo mkubwa wa magonjwa.

Mapungufu katika ushuru wa vinywaji vyenye sukari

Ripoti zinaonyesha kuwa angalau nchi 116 hutoza ushuru kwa vinywaji vyenye sukari, hasa soda. 

Hata hivyo, bidhaa nyingi zenye sukari nyingi bado hazitozwi kodi, zikiwemo juisi za matunda asilimia 100, vinywaji vya maziwa vilivyoongezwa sukari, na kahawa au chai zilizo tayari kunywa.

Ingawa asilimia 97 ya nchi hutoza ushuru kwa vinywaji vya kuongeza nguvu, WHO inasema kiwango hiki hakijabadilika tangu mwaka 2023, ikionyesha kusimama kwa maendeleo. 

Kwa wastani, kodi ya vinywaji vyenye sukari inachangia takriban asilimia 2 tu ya bei ya rejareja ya soda ya kawaida kiwango kilicho chini sana kuathiri matumizi.

Mstari wa chupa zenye rangi nyingi za maji ya matunda zilizowekwa kwenye friji kwenye duka kubwa.

© Unsplash/Thomas Park

Vinywaji vilivyojaa sukari vimewekwa kwenye maduka makubwa.

Pombe inaendelea kuwa nafuu licha ya hatari zilizo wazi

Ripoti tofauti ya WHO imebaini kuwa nchi 167 hutoza ushuru wa aina fulani kwa vileo, huku nchi 12 zikikataza pombe kabisa. 

Pamoja na hilo, pombe imekuwa nafuu zaidi, au bei kubaki bila kubadilika, katika nchi nyingi tangu mwaka 2022.

Mvinyo hauwekewi ushuru katika takriban nchi 25, nyingi zikiwa Ulaya, licha ya kile WHO ilichoeleza kuwa “hatari za kiafya zilizo wazi na zilizothibitishwa.”

Kwa mujibu wa Dkt. Etienne Krug, Mkurugenzi wa Idara ya WHO ya Vigezo vya Afya, Uhamasishaji na Kinga “Pombe inapokuwa nafuu zaidi, huongeza vurugu, majeraha na magonjwa. Wakati sekta inanufaika, umma hubeba madhara ya kiafya na jamii hulipa gharama za kiuchumi.”

Kwa kiwango cha kimataifa, WHO imegundua kuwa wastani wa sehemu ya ushuru wa forodha bado ni mdogo, ukiwa karibu asilimia 14 ya bei ya bia na asilimia 22.5 kwa vinywaji vikali.

Uungwaji mkono wa umma na wito wa kuchukua hatua

WHO imesisitiza kuwa ushuru dhaifu unaendelea kuwepo licha ya uungwaji mkono mkubwa wa umma. 

Utafiti wa Gallup wa mwaka 2022 ulionesha kuwa watu wengi walioulizwa waliunga mkono kuongeza kodi kwa pombe na vinywaji vyenye sukari.

Shirika hilo linazitaka serikali kuongeza na kubuni upya kodi ya afya chini ya mpango wake mpya wa “3 kwa 35”, unaolenga kuongeza bei halisi za tumbaku, pombe na vinywaji vyenye sukari ifikapo mwaka 2035.

WHO imesema “Kuendelea kufanya bidhaa hizi kuwa ghali zaidi kwa muda si tu sera bora ya kifedha bali ni uwekezaji muhimu katika kulinda afya ya watu na kuokoa maisha.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *