
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitiza azma ya taifa hili ya kutetea mamlaka yake ya kitaifa dhidi ya uingiliaji wa kigeni.
Sayyid Abbas Araghchi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema hayo katika mazungumzo yake kwa njia ya simu na Sheikh Abdullah bin Zayed bin Sultan Al Nahyan, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati).
Katika mazungumzo yao hayo, wawili hao wamebadilishana mawazo kuhusiana na matukio ya kieneo na kimataifa Pamoja na masuala yanayohusiana na uhusiano wa pande mbili.
Katika mazungumzo hayo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Seyyed Abbas Araghchi akigusia machafuko ya hivi karibuni ya Iran ambayo yametokana na uchochezi wa baadhi ya magaidi wa utawala wa Kizayuni na Marekani na kuvurugwa maandamano ya amani ya umma amesisitiza kuwa, kumekuwepo utulivu kutokana na kuwa macho wananchi na vyombo vya usalama.
Araghchi ameashiria pia matamshi ya kichochezi ya viongozi wa Marekani ambayo yanahesabiwa kuwa ni uingiliaji wa wazi katika masuala ya ndani ya Iran na akasisitiza azma ya wananchi wa Iran ya kutetea mamlaka ya taifa na usalama wa nchi dhidi ya wa uovu na uingiliaji wowote wa kigeni.
Kwa upande wake, Sheikh Abdullah bin Zayed Al Nahyan, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa UAE, pia alisisitiza umuhimu wa mashauriano endelevu kati ya Tehran na Abu Dhabi na nchi za eneo hili, na hitajio la juhudi za pamoja ili kuimarisha utulivu na usalama wa kikanda. Afisa huyu wa Falme za Kiarabu, akizungumzia umuhimu wa mashauriano endelevu kati ya Tehran na Abu Dhabi na nchi za eneo hilo, aliona juhudi za pamoja kuwa muhimu ili kuimarisha utulivu na usalama katika Asia Magharibi.