Rabat, Morocco. Wenyeji wa mashindano ya Kombe la Mataifa Afrika (AFCON) 2025, Morocco wamefanikiwa kutinga fainali ya michuano hiyo baada ya kuichapa Nigeria kwa penalti 4-2 katika mchezo uliofanyika Rabat.

Baada ya sare ya bila kufungana kwa dakika 120, hatimaye mechi ilifikia kwenye hatua ya kupigiana penalti ndipo iliposhuhudiwa Super Eagles ikikosa mikwaju miwili wakati Simba wa Atlas ikikosa mkwaju mmoja.

Youssef En-Nesyri alifunga penalti ya ushindi baada ya Yassine Bounou kuokoa mikwaju miwili ya Samuel Chukwueze na Bruno Onyemaechi.

Hii inamaanisha Simba wa Atlas wamefikiwa kutinga fainali yao ya kwanza ya Afcon tangu 2004, huku wakitaka kuinua taji hilo kwa mara ya kwanza tangu 1976.

Morocco itakabiliana na Senegal katika fainali ya Jumapili, ambapo Simba wa Teranga wamefika hatua hiyo baada ya kuwachapa Misri  1-0 shukrani kwa bao la Sadio Mane kwenye kipindi cha pili.

Mzimu wa AFCON unavyomtafuna Salah

Ndoto ya mshambuliaji nyota wa Liverpool, Mohamed Salah, ya kutwaa taji la Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) imeendelea kuyeyuka baada ya Misri kuondolewa katika hatua ya nusu fainali na Senegal.

Katika mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Tangier Grand nchini Morocco, Senegal ilipata ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya Misri, huku bao pekee likifungwa na Sadio Mane dakika ya 12 kabla ya filimbi ya mwisho.

Matokeo hayo yameendeleza maumivu ya Salah katika mashindano ya AFCON, taji pekee kubwa linalokosekana kwenye kabati lake la mafanikio, licha ya kutwaa mataji mbalimbali akiwa na klabu yake ya Liverpool.

Misri ni taifa lililotwaa AFCON mara nyingi zaidi barani Afrika likifanya hivyo mara saba, lakini haijashinda taji hilo tangu mwaka 2010, kabla Salah hajaanza kuitumikia timu ya taifa.

“Nimeshinda karibu kila kitu. Hili ndilo taji ninalolisubiri.” Alinukuliwa Salah baada ya Misri kuifunga Ivory Coast katika robo fainali.

Hata hivyo, Mane ameendelea kuwa mwiba kwa Salah katika michuano ya kimataifa. Huu ni ushindi wa tatu mfululizo wa Mane dhidi ya Salah, baada ya awali kuifunga Misri katika fainali ya AFCON 2021 kupitia mikwaju ya penalti, na kisha Senegal kushinda mchezo wa mchujo wa kufuzu Kombe la Dunia 2022 nchini Qatar.

Licha ya wawili hao kuonekana kupeana mikono ya heshima kabla ya kuanza kwa mchezo, mvutano ulijitokeza uwanjani baada ya Salah kumfanyia Mane faulo mwishoni mwa kipindi cha kwanza, jambo lililosababisha malumbano katika benchi la ufundi kwa timu zote mbili.

Kwa matokeo hayo, Salah ataendelea kusalia Afrika, kwani Misri itacheza mchezo wa kuwania nafasi ya tatu dhidi ya Nigeria utakaopigwa Jumamosi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *