Dar es Salaam. Vodacom Tanzania imeendelea kuthibitisha ubora wake katika usimamizi wa rasilimali watu baada ya kutambuliwa tena kama Mwajiri Bora nchini kwa mara ya tisa mfululizo na Taasisi ya Top Employers.

Miongoni mwa sababu kuu zilizoifanya Vodacom kuendelea kushika nafasi ya juu ni sera thabiti za rasilimali watu zinazolenga kujenga mazingira jumuishi, yenye usawa na yanayowezesha wafanyakazi kukua kitaaluma na binafsi. Tathmini ya Top Employers ilifanyika katika maeneo 20 muhimu yakiwemo mkakati wa wafanyakazi, uongozi, uajiri, ustawi wa wafanyakazi na usawa wa kijinsia.

Vodacom imeweka mkazo mkubwa katika ustawi wa wafanyakazi wake kwa kutoa manufaa yanayowahusu wao na familia zao, sera rafiki za likizo, pamoja na mifumo ya kazi inayoruhusu kufanya kazi kwa urahisi popote. Hatua hizi zimeongeza kuridhika kwa wafanyakazi na kuchochea utendaji bora kazini.

Sababu nyingine ni uwekezaji katika kukuza vipaji na ujuzi, hasa kwa kuandaa wafanyakazi kwa kazi za baadaye. Kupitia maboresho ya Thamani ya Ajira kwa Wafanyakazi (Employee Value Proposition) mwaka 2025, Vodacom imeongeza fursa za mafunzo, ukuaji wa taaluma na maendeleo ya uongozi kwa wafanyakazi wa ngazi zote.

Kampuni hiyo pia imejipambanua kwa kuhamasisha ushiriki wa wanawake katika sekta ya teknolojia, kupitia programu maalumu zinazolenga kuongeza usawa wa kijinsia na kutoa fursa sawa za maendeleo.

Juhudi hizo zimeifanya Vodacom kutajwa kama mwajiri anayejali na kuthamini mchango wa kila mfanyakazi.

Akizungumzia mafanikio hayo, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu wa Vodacom Tanzania, Vivienne Penessis, amesema mafanikio hayo yanatokana na dhamira ya dhati ya kampuni kuhakikisha wafanyakazi wanajihisi kuthaminiwa na kuungwa mkono katika mazingira yao ya kazi.

Mbali na ndani ya kampuni, Vodacom imepanua mchango wake kwa jamii kwa kuwekeza katika programu za kukuza vipaji vya vijana kama Graduate Trainee Program, Code Like a Girl na Digital Skills Hub. Programu hizo zimechangia kuandaa nguvu kazi yenye ujuzi kwa uchumi wa kidijitali na kuongeza mvuto wa kampuni kama mwajiri wa kuaminika.

Aidha, mwelekeo wa Vodacom wa kujiimarisha kama taasisi ya kidijitali inayotumia teknolojia za kisasa ikiwemo akili mnemba (AI) umechangia kuongeza ufanisi wa kazi na kuwajengea wafanyakazi uwezo wa kuendana na mabadiliko ya soko la ajira.

Kwa ujumla, mchanganyiko wa uongozi bora, sera rafiki kwa wafanyakazi, uwekezaji katika teknolojia na vipaji, pamoja na utamaduni chanya wa kazi unaoweka wateja mbele, umeifanya Vodacom Tanzania kuendelea kung’ara na kutambuliwa kama Mwajiri Bora nchini kwa miaka mfululizo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *