
Dar es Salaam. Singida Black Stars imetangaza kuwa beki wake Nickson Kibabage amejiunga na Simba kwa uhamisho wa bure baada ya makubaliano baina ya pande hizo.
Taarifa iliyotolewa na Singida Black Stars leo, imefafanua kuwa klabu hiyo imeridhia Kibabage ajiunge na Simba kwa faida ya mchezaji husika.
“Singida Black Stars inapenda kuufahamisha umma kuwa imekubali maombi kutoka kwa uongozi wa Klabu ya Simba ya kumruhusu mchezaji Nickson Kibabage kujiunga na klabu hiyo.
“Baada ya majadiliano, uongozi umeamua kumtoa mchezaji huyo bila malipo.
Singida Black Stars inaamini katika falsafa ya uendelezaji vipaji hasa kwa wachezaji wazawa. Uongozi wa klabu umeona hii ni fursa nzuri kwa mchezaji mzawa kwa kuwa Simba SC inashiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Nickson Kibabage ni Mchezaji wa Timu ya Taifa.
“Tunamtakia kila la kheri Nickson Kibabage katika safari yake mpya ya soka nje ya Singida Black Stars,” imefafanua taarifa ya Singida Black Stars.
Beki huyo wa kushoto alikuwa na mkataba wa miezi sita ambao alibakiza na Singida Black Stars ambayo ilimnasa katika dirisha kubwa la usajili akitokea Yanga.
Mbali na Yanga na Singida Black Stars, Kibabage pia amewahi kuzitumikia Singida Big Stars, Mtibwa Sugar na Difaa Hassan El Jadida ya Morocco.
Beki huyo wa kushoto anayemudu pia kucheza nafasi ya winga, anakuwa mchezaji wa pili kutoka Singida Black Stars kuitumikia Simba msimu huu.
Katika dirisha kubwa la usajili kabla ya msimu wa 2025/2026 kuanza, Singida Black Stars ilimruhusu mshambuliaji wake Jonathan Sowah.