
Nahodha wa timu ya Taifabya Nigeria ‘Super Eagles’, Wilfred Ndidi ameliomba Shirikisho la Mpira wa Miguu la Nchi yake (NFF), kutomtimua Kocha Mkuu wa timu hiyo Eric Chelle.
Ndidi amesema kuwa ni muhimu kwa Chelle kubakia katika nafasi hiyo ili kuendeleza kile alichokianzisha katika Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 zinazoendelea Morocco.
Hatima ya Chelle iko kwenye mabano kufuatia timu hiyo kufungwa na Morocco kwa mikwaju ya penalti 4-2 katika mechi ya nusu fainali ya mashindano hayo.
Kabla ya kuanza kwa AFCON 2025, NFF ilimuwekea Chelle lengo la kuifikisha timu yao ya Taifa hatua ya fainali lakini hilo limeshindwa kutimia na kumetanda wasiwasi kuwa anaweza kuonyeshwa mlango wa kutokea.
Kocha huyo mwenye umri wa miaka 48 raia wa Mali, ameonekana kutamani kubakia katika kibarua chake lakini amejulishwa kwamba anapaswa kusubiria uamuzi wa NFF.
Lakini Chelle anaonekana kushinda imani ya nyota wa kikosi hicho akiwemo Ndidi ambaye amefichua wazi kuwa wanatamani kuona wanabaki na kocha huyo.
“Kiujumla nataka tubaki na kocha. Tunatakiwa kujikita katika muendelezo katika pointi ya sasa,” amesema Ndidi.
Baada ya kushindwa kutinga hatua ya fainali, Chelle angalau anaweza kujipooza na medali ya mshindi wa tatu ikiwa ataiongoza Nigeria kuibuka na ushindi katika mechi ya kuwania mshindi wa tatu itakayochezwa kesho Jumamosi, Januari 17, 2026.