Dar es Salaam. Unalikumbuka kundi la TMK Wanaume Family ambalo lilitamba kwa staili yao ya uchezaji wa ‘Mapanga Shaa’?
Jikumbushe, kundi hilo lilikuwa likiundwa na wasanii maarufu kama Juma Nature, Chege, Mh Temba, Stiko, KR, Luteni Kalama na wengine wengi.
Kundi hilo lilifanya vizuri na nyimbo zake kama ‘Nyumbani ni Nyumbani’, ‘Ndiyo zetu’ na nyingine kibao. Licha ya kupendwa na wengi ilipofika mwaka 2006 lilisambaratika na hatimaye kuzaliwa makundi mawili TMK Wanaume Halisi na ‘TMK Wanaume Family.
Aliyekuwa meneja wa kundi hilo Saidi Fela aliwahi kutoa historia ya kundi kwamba lilizaliwa rasmi mwaka 2002 jijini Mwanza na aliyetoa wazo la kuundwa kundi hilo alikuwa ni MC wa onyesho ambaye alikuwa ni mwigizaji maarufu wa Kaole kipindi hicho Swebe. Baada ya kurudi Dar es Salaam walifikiria jina la kundi na hatimaye wakaamua waliite Wanaume Family.
Kwanini Wanaume Family?
Jina la Wanaume lilitokana na tabia ya vijana ambao walikuwa wakikaa maeneo ya Uwanja wa Taifa wa zamani kusema wanaume! Wanaume hao! pale wanapoona polisi wanafanya doria uwanjani kutafuta vibaka waliokuwa wakijificha maeneo yanayozunguka uwanja huo.
Hivyo basi kwa sababu wasanii hao walikuwa wakikutana maeneo ya hapo Uwanja wa Taifa wa zamani, jina Wanaume lilikuwa maarufu kwao wakaamua kutumia jina hilo TMK Wanaume Family.
Utamu wa muziki wa kundi hilo ulisababisha upinzani wa kimuziki na kundi lingine la East Coast lililokuwa na wasanii kama Ay, MwanaFa, GK na wengineo.
TMK Wanaume Family walifanikiwa kutoa album moja iliyokuwa inaenda kwa jina la ‘Ndiyo zetu’ ambayo ndani ilikuwa na wimbo wa ‘Nyumbani Nyumbani’ uliochukua tuzo za Tanzania za Kilimanjaro kama Wimbo Bora wa Hip Hop.
Said Fella aliwahi kusema yeye alikuwa ana nia ya kujenga lakini wakati kundi hilo lilipoanza kupata neema ya mafanikio ndiyo likasambaratika, huku yeye akibaki na wasanii kama Chege na Mh Temba, YP na Y dash ingawa baadaye nao waliondoka. TMK Wanaume Halisi ikabaki na wasanii kama Juma Nature, Luteni Kalama, KR na wengineo.