
Taarifa za awali zinasema kuwa watu wasiopungua wanane wamepoteza maisha na wengine zaidi ya ishirini wamejeruhiwa baada ya moto mkubwa kuzuka katika eneo la Makina la makazi duni ya watu huko Kibera, Kaunti ya Nairobi nchini Kenya.
Vyombo vya habari vya ndani na nje ya Kenya ikiwemo TV47 vimetangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, moto huo umetetekeza eneo hilo lenye watu wengi na kusababisha uharibifu mkubwa wa mali huku familia nyingi zikiendelea kuomboleza kutokana na kupoteza makazi na wapendwa wao.
Watoa misaada ya dharura wamekimbilia eneo hilo na kupeleka maiti kwenye vyumba vya kuhifadhia maiti na kwa wale waliojeruhiwa wamepelekwa kwenye Hospitali ya Taifa ya Kenyatta kwa matibabu. Hadi wakati tunaandaa taarifa hii, uchunguzi kuhusu chanzo cha moto huo ulikuwa bado unaendelea.
Taarifa za awali zinasema kuwa zaidi ya nyumba 40 zimeteketea kwa moto, huku tathmini hasa ya hasara iliyosababishwa na moto huo ikitarajiwa kutolewa baadaye.
Wakazi wenye majonzi wa eneo hilo la mabanda wameitaka serikali ichukue hatua za haraka za kuwasaidia wahanga wa moto huo, huku mmoja wa wakazi hao akisema kuwa, kwa uchache katika kila nyumba kuna watu watano, na nyumba zote zilizoungua ni 40 hivyo kuna uwezekano wa idadi ya wahanga ikaongezeka.
“Sasa tunaomba serikali mukuje musaidie watu, juu kuna manyumba tuseme forty hapa na familia wako ndani unapata familia moja wako watu watano ndani,” amesema mmoja wa wakazi wa eneo hilo alipohojiwa na TV47.
Wakazi wa eneo hilo wamelalamika kwamba manispaa wa Jiji la Nairobi kwa mara nyingine imewavunja moyo kwani maafisa wa Zima Moto walichelewa sana kufika kwenye eneo la tukio.