Dar/Mikoani. Kadri Tanzania inavyoendelea kuwekeza katika michezo, mjadala wa miundombinu jumuishi unaibuka ili kuhakikisha hakuna anayebaki nje ya uwanja kwa sababu ya ulemavu wake.

Watu wenye ulemavu nchini Tanzania wanakabiliwa na changamoto ya kuingia na kutumia viwanja vya michezo kutokana na miundombinu isiyozingatia mahitaji yao, hali inayowatenga katika shughuli za kijamii licha ya kuwepo kwa sheria zinazoelekeza ushirikishwaji na usawa.

Uchunguzi wa miezi mitatu uliofanywa na Mwananchi katika mikoa ya Dar es Salaam na Arusha umebaini katika viwanja vingi vya michezo, hususani vinavyotumika kwa mechi za soka, mazingira hayajaandaliwa kuwahudumia watu wenye ulemavu wa viungo, uoni au usikivu.

Ngazi ndefu zisizo na njia mbadala, kukosekana kwa miteremko maalumu, vyoo visivyo rafiki na maeneo yasiyo na nafasi ya vitimwendo ni miongoni mwa vikwazo vinavyowalazimu baadhi ya mashabiki kubaki nje ya viwanja au kuacha kabisa kuhudhuria michezo.

Watu wenye ulemavu wakiwa uwanja wakishuhudia mchezo wa mpira wa miguu. Picha na Maktaba

Baadhi ya watu wenye ulemavu wanasema hali hiyo inawanyima haki ya kufurahia michezo kama Watanzania wengine, hususani soka ambalo ni mchezo unaopendwa zaidi nchini na unaovutia maelfu ya mashabiki.

SHERIA ZINASEMAJE?

Kisheria, Tanzania ina mifumo inayolinda haki za watu wenye ulemavu. Sheria ya Watu Wenye Ulemavu ya mwaka 2010 inatamka wazi wajibu wa Serikali, taasisi za umma na binafsi kuhakikisha miundombinu ya majengo ya umma, ikiwemo viwanja vya michezo, inakuwa rafiki na inayoweza kutumiwa na watu wote bila ubaguzi.

Sheria inasisitiza upatikanaji sawa wa huduma za kijamii, burudani na michezo, sambamba na wajibu wa kufanya marekebisho stahiki pale inapobidi.

Vilevile, Tanzania ni mwanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Watu Wenye Ulemavu, unaolazimisha nchi wanachama kuhakikisha ushiriki kamili wa watu wenye ulemavu katika maisha ya kijamii, ikiwemo michezo na burudani.

Mkataba huu ulipitishwa mwaka 2006 na Tanzania iliusaini Machi, 2007, kisha ikauridhia Novemba. 2009.

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pia inalinda haki ya usawa na kutobaguliwa, ikimaanisha kuwa raia wote wanapaswa kupata fursa sawa za kushiriki katika shughuli za kijamii, zikiwamo michezo na burudani.

Kwa maneno mengine, kisheria, watu wenye ulemavu wana haki kamili ya kuingia viwanja vya michezo, kukaa kwa usalama na kushiriki kama mashabiki au wanamichezo bila vikwazo vya kimazingira.

Watu wenye ulemavu wakiwa uwanja wakishuhudia mchezo wa mpira wa miguu. Picha na Maktaba

Hata hivyo, utekelezaji wa sheria hizo bado unaonekana kuwa dhaifu, hasa katika sekta ya michezo. Miradi ya ujenzi au ukarabati wa viwanja imekuwa ikilenga zaidi mahitaji ya kibiashara, usalama wa jumla na hadhi ya kimataifa, huku masuala ya watu wenye ulemavu yakipewa uzito mdogo.

HALI HALISI VIWANJANI

Uchunguzi wa Mwananchi katika viwanja vikiwamo vya KMC Complex, Azam Complex na Uwanja wa Uhuru, vilivyopo jijini Dar es Salaam, umebaini licha ya kutumika kwenye michezo ya Ligi Kuu Bara na hata mashindano mengine, havina sifa ya kuwahudumia watu wenye ulemavu.

Tofauti na hivyo, Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, uliopo mkoani Arusha, una nafuu ukiwa na njia mbili zinazoweza kutumiwa na watu wenye ulemavu kwenda majukwaa ya VIP lakini huduma hizo zikikosekana kwenye jukwaa kuu la VVIP na mengine ya pembeni.

Viwanja vingi vilivyojengwa kabla ya mwaka 2000 havitoi fursa kwa watu wenye ulemavu, huku vile vilivyojengwa baada ya hapo vina baadhi ya huduma lakini siyo zote.

Uwanja wa Benjamin Mkapa, ulioko Dar es Salaam, ulioanza kujengwa mwaka 2005 na kukamilika 2007, ndiyo mkubwa zaidi nchini Tanzania, wenye uwezo wa kuchukua mashabiki 60,000.

Tofauti na viwanja vingine, huu una huduma nyingi kwa watu wenye ulemavu, ukiwa na njia za kutosha kwa ajili yao na una lifti za kwenda jukwaa la VVIP.

Hata hivyo, uwanja huu unakosa njia za watu wenye ulemavu kwenda majukwaani kwa ndani ili kufikia sehemu za kukaa.

Kutokana na viwanja vingi kukosa njia maalumu kwa watu wenye ulemavu, imekuwa adha kwao wakijikuta wakipishana na watu wengine, hivyo kuhatarisha usalama wao wanapoingia na kutoka viwanjani.

“Unapofika uwanjani unagundua haukuzingatiwa kabisa. Hata ukiingia, huwezi kukaa mahali panapokupa usalama na mwonekano mzuri wa mchezo,” anasema mmoja wa mashabiki wenye ulemavu wa viungo, jijini Dar es Salaam.

Imebainika katika uchunguzi kuwa, kutokana na adha wanayopitia, baadhi ya mashabiki wamekuwa wakiwatumia watu wenye ulemavu kuingia uwanjani ili kukwepa malipo ya viingilio, wakijitolea kusukuma baiskeli zao ili kupita kwenye geti kuu la kuingia uwanjani linalotumiwa na magari.

Watu wenye ulemavu wakiwa uwanja wakishuhudia mchezo wa mpira wa miguu. Picha na Maktaba

Kutokana na geti hilo kutokuwa rasmi kwa ajili ya mashabiki, wapo wanaozuiwa, hivyo kuishia kupata changamoto viwanjani.

Ili kuwawezesha Kwenda kukaa kwenye viti, baadhi ya mashabiki kujitolea kuwabeba wenye ulemavu, hususani wakati wa kupanda ngazi.

Amiri Said, mwenye ulemavu wa viungo, mkazi wa jijini Arusha, anasema aliwahi kuumizwa akiwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, baada ya kuzuka vurugu za mashabiki wakati wa fainali za Kombe la Azam Federation kati ya Yanga na Coastal Union.

Anaeleza kutokana na vurugu hizo alichubuka mikononi na simu yake iliharibika, hivyo akaacha kwenda uwanjani akihofia kuumizwa kwani hushindwa kwenda kwenye jukwaa ambalo atakaa kwa usalama.

“Unaona yale majukwa ya pembeni (anaonyesha) ukiingia kwa upande wa nyuma, Polisi wanakuzuia, hivyo ilikuwa ngumu kufika kwenye jukwaa ambalo tulitakiwa kukaa,” anasema na kuongeza:

“Wenzangu walinisaidia nikakaa jukwaa ambalo hatukuwa tumepangiwa, vurugu zilipotokea niliumizwa na simu ikavunjika. Sasa nabaki nyumbani kuangalia mechi kwenye televisheni.”

Imebainika pia, vyoo vilivyopo uwanjani havikidhi mahitaji ya wenye ulemavu, hivyo baadhi yao wakilazimika kukanyaga au kushika mazingira machafu yaliyopo vyooni hali inayohatarisha afya zao.

Albert Kiwela, shabiki wa soka wenye ulemavu wa viungo, mkazi wa jijini Dar es Salaam, anasema viwanja vya soka vimeshindwa kuzingatia kuwapa huduma stahiki za vyoo, hivyo hulazimika kukanyaga maji machafu wakati akiingia chooni.

“Sisi tuna haki ya kupata huduma sahihi, kuingia kwetu viwanjani ni mpaka tusaidiwe na watu bado tena tukifika huku ndani tuwe hatarini kupata maradhi,” anasema.

WAMESEMAVYO MAMENEJA WA VIWANJA

Meneja wa Uwanja wa KMC, Hussein Kitundura, anakiri kuwapo changamoto za huduma kwa watu wenye ulemavu uwanjani hapo, akieleza bado wanaendelea kuuboresha.

“Uwanja haujakamilika kama ambavyo Halmashauri ya Kinondoni inavyokusudia, lakini kutokana na mahitaji ulianza kutumika. Bado kuna awamu za ujenzi zinaendelea,” amesema na kuongeza:

“Lengo la Halmashauri ya Kinondoni ni kuona uwanja huu unakidhi mahitaji yote kwa watumiaji wa makundi yote.”

Amesema halmashauri imekuwa ikikutana na wadau mbalimbali ambao hutoa mapendekezo ya kuboresha uwanja huo ili uwe wa kisasa zaidi.

Akizungumzia Uwanja wa Sheikh Amri Abeid uliojengwa mwaka 1975, Meneja wa uwanja huo, Emmanuel Loi, anakiri kuwepo upungufu katika utekelezaji wa sheria inayolenga watu wenye ulemavu.

Anasema maboresho ya uwanja huo kuelekea Fainali za Mataifa Afrika mwaka 2027, zitakazofanyika nchini mahitaji ya watu wenye ulemavu yatazingatiwa na kila kitu kitakuwa sawa.

“Uwanja huu ulijengwa zamani hata maboresho hayakuwa yamefanyika. Lakini kuna maeneo mawili yenye njia maalumu za kupita watu wenye ulemavu. Zilijengwa baada ya kuona wakiingia na kukaa ndani ya uzio jambo ambalo si salama,” anasema.

Anaeleza viti vya mbele ni maalumu kwa ajili ya watu wenye ulemavu.

Hata hivyo, anasema hakuna njia kwa ajili ya wenye ulemavu kwenda eneo la VVIP kwani kuna ngazi pekee ambazo haziwapi fursa ya kulifikia.

“Tutakuwa na maboresho ya uwanja huu hivi karibuni, Serikali imetenga fedha za kutosha ambazo zitakwenda kuufanyia maboresho makubwa kwa ajili ya Fainali za Mataifa Afrika, kupitia hayo tutazingatia mahitaji ya watu wenye ulemavu,” amesema.

Kadri Tanzania inavyoendelea kuwekeza katika michezo, mjadala wa miundombinu jumuishi unaibuka ili kuhakikisha hakuna anayebaki nje ya uwanja kwa sababu ya ulemavu wake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *