Dodoma. Wateja wa Vodacom Tanzania katika Mkoa wa Dodoma na mikoa ya jirani ya Kanda ya Kati wanatarajiwa kunufaika zaidi na huduma za mawasiliano kufuatia uzinduzi wa duka kubwa jipya mkoani humo.
Duka hilo, ambalo limeboreshwa kwa miundombinu na mifumo ya kisasa, linatarajiwa kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wateja kwa wakati mmoja, tofauti na ilivyokuwa awali.
Akizungumza wakati wa uzinduzi, Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania, Philip Besiimire amesema duka hilo limezingatia mahitaji ya wateja wote, ikiwemo wale wenye mahitaji maalumu kama viziwi, watu wenye ulemavu wa miguu na macho, huduma ambayo haikuwepo katika duka la awali.
Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania, Philip Besiimire (kushoto) akitazama moja ya simu zinazouzwa ndani ya duka jipya kubwa la Vodacom mkoani Dodoma baada ya kulizindua jana. Wanaoshuhudia ni wafanyakazi wa duka hilo.
Amesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha kila mteja anapata huduma bila vikwazo.
Baadhi ya wateja waliohudhuria uzinduzi huo wamesema duka hilo ni mkombozi kwao, wakieleza kuwa ukubwa wake na mpangilio wa kisasa utapunguza msongamano na muda wa kusubiri huduma.
Mmoja wa wateja hao, amesema awali walilazimika kusubiri kwa muda mrefu kutokana na nafasi ndogo ya duka la zamani, lakini kwa sasa matarajio ni kupata huduma kwa haraka na kwa ubora zaidi.