
Akijibu tukio hilo la kushtua, Mkuu wa UNRWA, Philippe Lazzarini, amelieleza kama “shambulio lisilo na kifani” dhidi ya Umoja wa Mataifa, ambao majengo yake yanalindwa chini ya sheria za kimataifa.
“Tingatinga zimengia katika eneo la jengo hilo na kuanza kubomoa majengo yaliyokuwa ndani yake, huku wabunge na mtu wa serikali wakishuhudia.” Amendika Lazarrini katika ukurasa wake wa X na baadaye taarifa hiyo kuchapishwa na UNRWA.
Kamishna Mkuu wa UNRWA ameeleza kwamba, “hatua hiyo inawakilisha “kiwango kipya cha ukaidi wa wazi wa serikali ya Isreal, tena wa makusudi wa sheria za kimataifa, ikiwemo heshima na kinga ya Umoja wa Mataifa.”
Bwana Lazzarini ametahadharisha kwamba kitu kama hicho kinaweza kutokea kwa shirika au ujumbe wowote wa kidiplomasia “popote duniani,” na kwa hivyo, “Hili lazima liwe wito wa kuamka”.
“Hili ni matokeo ya moja kwa moja ya sheria iliyopitishwa na bunge la Israel mwezi Desemba, ambayo iliongeza nguvu kwa sheria zilizokuwepo za kupinga UNRWA zilizopitishwa mwaka 2024,” amesema Bwana Lazzarini.
Mnamo tarehe 14 Januari, majeshi ya Israel yaliingia katika kituo cha afya cha UNRWA Mashariki mwa Jerusalem na kuamuru kifungwe. Wakati wa tukio hilo, shirika lilisema wafanyakazi wake walikuwa “na hofu kubwa.”
Katika wiki zijazo, huduma za maji na umeme kwa vituo vya UNRWA zinatarajiwa kukatwa, ikiwemo majengo yanayotumika kwa huduma za afya na elimu.
Hapo awali, majengo ya UNRWA yalilengwa na wachomaji moto katikati ya “kampeni kubwa ya upotoshaji wa taarifa” dhidi yake inayofanywa na Israel, ameongeza Kamishna Mkuu wa UNRWA.
Haya yalitokea licha ya uamuzi wa Oktoba iliyopita wa mahakama kuu ya Umoja wa Mataifa, Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ), ambao ulisisitiza kuwa Israel ina wajibu “kusaidia shughuli za UNRWA, si kuzizuia au kuzifungia. Mahakama pia ilisisitiza kuwa Israel haina mamlaka juu ya Jerusalem Mashariki,” amebainisha Bwana Lazzarini.
“Kinachotokea leo kwa UNRWA kitatokea kesho kwa shirika lolote la kimataifa au ujumbe wa kidiplomasia, iwe katika Ardhi ya Palestina inayokaliwa au popote duniani,” ameendelea kusema. “Sheria za kimataifa zimekuwa zikishambuliwa kwa muda mrefu na sasa zinahatarisha kupoteza umuhimu wake kutokana na kukosekana kwa mwitikio kutoka kwa Nchi Wanachama.”
Hasira ya Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa
Akisisitiza wasiwasi huo, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Türk, naye kupitia Msemaji wake, leo ameeleza “hasira” yake kuhusu tukio hilo, ambalo linaashiria kuongezeka kwa kasi kwa mvutano kati ya mamlaka za Israel na UNRWA.
“Hili linaongeza kile ambacho tumekuwa tukiona kwa muda; kushambulia mashirika ya misaada na watendaji wa Umoja wa Mataifa wanaojaribu kusaidia,” amesema leo jijini Geneva, Uswisi, Ravina Shamdasani, msemaji wa Volker Türk.