Korea. Umaarufu katika tasnia ya burudani mara nyingi huonekana kama kilele cha mafanikio, lakini kwa mastaa wengi, huwa na mitego mingi.
Tukio moja la kashfa linaweza kubadili kabisa mwelekeo wa maisha na kazi ya msanii, hasa katika jamii kama ya Korea Kusini ambako maadili, taswira safi na nidhamu vina nafasi kubwa mbele ya umma.
Skendo zinazohusisha dawa za kulevya, tuhuma za kingono, ukwepaji kodi au migogoro ya kimaisha zimewahi kuwageuza mastaa kutoka kilele cha umaarufu hadi kutengwa na tasnia.
Mifano ya mastaa wa Kikorea waliotamba katika tamthilia na filamu mbalimbali duniani kutoka Korea Kusini waliotikiswa na skendo ni pamoja na Yoo Ah-in, ambaye taaluma yake ilisimama baada ya kesi ya matumizi ya dawa za kulevya, Park Yoo-chun aliyepoteza kabisa soko la Korea kutokana na mfululizo wa kashfa na wengineo.
Hali kama hiyo haipo Korea pekee barani Ulaya, mastaa kadhaa pia wamewahi kuyumba au kupoteza hadhi zao kutokana na skendo mbalimbali.
Mfano wa karibu ni nguli wa muziki Marekani, Sean Combs ambaye yuko gerezani akikabiliana na kifungo cha miezi 50 jela kwa makosa ya usafirishaji haramu wa watu. Wengine Kevin Spacey alikuwa muigizaji mkubwa Uingereza lakini tuhuma za unyanyasaji wa kingono zilimweka kando na tasnia.
Ipo mifano mingi lakini Mwananchi inakuchambulia baadhi ya wasanii wa Korea ambao skendo mbovu zimewafanya wakae pembeni na tasnia na kuwaharibia kabisa karia yao mbela ya mashabiki.
1. YOO AH-IN
Februari 2023 Polisi wa Korea Kusini walianza uchunguzi rasmi dhidi ya muigizaji huyo kuhusu matumizi ya dawa za kulevya.
Mei mwaka huo huo alikamatwa rasmi na kuwekwa rumande. Mahakama ilimhukumu kifungo cha mwaka mmoja na kifungo hicho kimebadilishwa kuwa hukumu iliyosimamishwa na muda wa jaribio wa miaka miwili.
Baada ya shutuma hizo Yoo hakupata madili ya kuigiza na aliondolewa kwenye tamthilia ya Hellbond Season 2 ambayo alikuwepo kama mmoja wa wahusika muhimu.
Alikuwa miongoni mwa waigizaji bora Korea na baadhi ya kazi alizowahi kufanya zikampa umaarufu mkubwa ni pamoja na Secret Love Affair (2014), Six Flying Dragons (2015/16), Chicago Typewriter (2017),Burning (2018), Hellbound (2021) na nyinginezo.
2. O YEONG-SU
Ni mwigizaji mkongwe alizaliwa mwaka 1944 Korea Kusini na alianza kazi ya uigizaji mwaka 1963 ni miongoni mwa mastaa waliokuwa wanafuatiliwa.
Novemba 25, 2022, waendesha mashtaka wa Suwon walitangaza O amefunguliwa mashtaka ya utovu wa nidhamu ya kingono dhidi ya mwanamke mmoja mwaka 2017.
Alishtakiwa kwa matukio kadhaa ya utovu wa nidhamu wa kingono, ikiwemo kumkumbatia mwanamke huyo bila ruhusa, kutoa maneno machafu ya kingono, kulala naye na kumbusu bila ridhaa, katika matukio tofauti tofauti. Ingawa tukio hilo alilifanya mwaka 2017 lakini alikamatwa 2022.
Wakati wa kesi yake mwezi Februari 2024, upande wa mashtaka uliomba adhabu ya kifungo cha mwaka mmoja jela, lakini O alikana mashtaka yote mwezi mmoja baadae alipatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo cha miezi minane.
Baada ya mashtaka na hukumu hiyo, O aliondolewa kwenye mfululizo wa tamthilia ya Squid Game na akapigwa marufuku kuonekana kwenye vituo vikuu vya utangazaji Korea Kusini.
Hata hivyo, baada ya kukata rufaa, mwezi Novemba 2025, O aliachiliwa huru akaondolewa mashtaka, mahakama ikasema hakukuwa na ushahidi wa kutosha na ikaeleza pia kuna uwezekano kumbukumbu za mlalamikaji kuhusu tukio hilo zilipotoshwa na zilipita kwa muda.
Alikuwa maarufu kwenye Squid Game, lakini kesi za unyanyasaji zilimnyima fursa nyingi za kazi, licha ya kufutiwa kesi kwa rufaa bado hajaonekana kideoni.
3. PARK YOO-CHUN
Mkali huyo alianza kazi mwaka 2003 kama mwanachama wa kundi maarufu la muziki la K-pop TVXQ, kabla ya kuondoka na kuunda kundi JYJ mwaka 2010.
Kupitia JYJ alijijengea umaarufu mkubwa Asia kama mwimbaji na rasmi akaingia kwenye uigizaji mwaka 2010 akijipata sifa kubwa kwa uwezo wake wa kuigiza na haiba yake.
Kama mwimbaji Yoo-chun alitoa baadhi ya ngoma zilizopendwa na mashabiki, ikiwemo ‘Found You’, ‘Get Out’, ‘I Love You’ na nyimbo za kundi la JYJ kama ‘In Heaven’ na Back Seat pia alishiriki katika tamthilia maarufu kama Sungkyunkwan Scandal (2010), Rooftop Prince (2012), Missing You (2012), na The Girl Who Sees Smells (2015).
Thamani yake ilianza kushuka mwaka 2016 alipotuhumiwa kuwafanyia unyanyasaji wa kingono wanawake wanne tofauti alikamatwa lakini baadae aliachiwa kwa kukosekana ushahidi wa kutosha.
Miaka mitatu baadae Park Yoo-chun alikamatwa kwa tuhuma za kununua na kutumia madawa ya kulevya, pamoja na tuhuma za kujaribu kuharibu ushahidi kabla ya kipimo cha dawa.
Baada ya kukutwa na mashtaka, wakala wake akasitisha mkataba wake na kutangaza kujiondoa kwenye tasnia ya burudani. Alipatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo cha miezi kumi.
Desemba 14, 2023, Yoo-chun alitajwa kwenye orodha ya wadaiwa wa kodi ya Huduma ya Taifa ya Kodi, akituhumiwa kwa ukwepaji wa kodi aliokuwa anadaiwa kiasi cha zaidi Milioni 700 ya Kitanzania.
4. LEE SEUNG-GI
Alianza kutambulika kama mwanamuziki ya nyimbo kama Debut, Because You’re My Woman, Will You Marry Me, Return na The Ordinary Man, ambazo ziliimarisha umaarufu wake Korea na Asia.
Kama muigizaji, alicheza kwenye tamthilia maarufu kama Brilliant Legacy (2009), My Girlfriend Is a Gumiho (2010), The King 2 Hearts (2012), Gu Family Book (2013), You’re All Surrounded (2014), A Korean Odyssey (2017–2018), Vagabond (2019), Mouse (2021), na The Law Cafe (2022) akipata umaarufu mkubwa Asia.
Nyota huyo pia amepata tuzo mbalimbali ikiwemo Four Mnet Asian Music Awards, five Seoul Music Awards, Two KBS Drama Awards, eight SBS Drama Awards na nyinginezo.
Hakuwahi kuhusika moja kwa moja na kashfa, lakini mwaka 2023–2024 jina lake liliingia kwenye mjadala mkubwa baada ya baba yake mkwe kuhusishwa na kesi ya utapeli katika soko la hisa.
Ingawa tukio hilo halikumhusu kisheria, baadhi ya wananchi na mashabiki walimkosoa kwa kutokuchukua tahadhari mapema, jambo lililoathiri kwa kiasi fulani taswira yake kwa umma.