Akihutubia Jukwaa hilo amesema uaminifu duniani hauwezekani bila kujitolea kwa misingi ya pamoja na kuheshimu ukweli.
Amekumbusha kuwa katika nyakati za kawaida, taasisi za mfumo wa ushirikiano wa kimataifa, hasa Umoja wa Mataifa, zilifanya kazi kama “mpatanishi” kusaidia nchi kuaminiana.
Hata hivyo, mwanadiplomasia huyo ameongeza kuwa dunia ya leo haiishi tena katika “nyakati za kawaida”.
Muonekano wa Mkutano wa Kila Mwaka wa Jukwaa la Ulimwengu la Uchumi wa 2026 huko Davos-Klosters, Uswisi
Dunia iko katika hatua ya mabadiliko
Baerbock amesema kuwa tayari wakati wa ufunguzi wa kikao cha 80 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwezi Septemba mwaka jana, uliweka bayana kwamba “dunia imesimama njiani panda,” ikikabiliwa na idadi ya juu kabisa ya migogoro, ikiwemo “takriban miaka minne ya uchokozi unaofanywa na mwanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama dhidi ya jirani yake ambao ni ukiukwaji wa wazi wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa.”
Ameongeza kuwa “Umoja wa Mataifa hauko tu chini ya shinikizo, bali uko chini ya shambulio la moja kwa moja”.
Ukweli na sheria kama msingi wa uaminifu
Akizungumza kuhusu haja ya kupambana na taarifa potofu, amemnukuu mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel, Maria Ressa: “Bila ukweli wa mambo, hakuna ukweli. Bila ukweli, hakuna uaminifu.” Kwa mujibu wa Baerbock, taarifa potofu zinatumika kama silaha katika dunia ya leo, na akili mnemba inaendelea kufifisha mpaka kati ya ukweli na uongo.
Ameongeza kuwa asilimia 96 ya video bandia au deepfakes zote ni za kingono na zinawalenga wanawake.
Pia ametetea ulimwengu unaoongozwa na sheria. Katika muktadha huo, ametaja hali inayohusu Greenland, ambayo Marekani inadai kupewa udhibiti wake. Baerbock amesisitiza kuwa hakuna maslahi ya kijiografia yanayoweza kuvuka haki za mamlaka ya wakazi wake kama raia wa Denmark, Muungano wa Ulaya na NATO.
“Huwezi kushinda medali ya dhahabu kama hufuati sheria. Utatolewa kwenye mashindano. Na hakuna mwekezaji atakayewekeza katika dunia ambayo sheria zake hazitabiriki,” amesema, akikumbusha kuwa dunia isiyo na sheria tayari imeshasababisha maafa.
Msaada kwa mfumo wa ushirikiano wa kimataifa
“Kulinda mfumo wa kimataifa unaozingatia sheria si ujinga, bali ni maslahi ya busara ya binafsi,” amesisitiza Rais wa Baraza Kuu.
Baerbock amesema kuwa uaminifu hupatikana kwa wale wanaotetea misingi hata inapokuwa vigumu, wanaochukua hatua licha ya gharama kubwa, na wanaosema ukweli pale ambapo ingekuwa rahisi zaidi kukaa kimya.
Katika hitimisho lake, Rais huyo wa Baraza Kuu ametoa wito wa kuundwa kwa muungano wamataifa baina ya kanda, biashara na viongozi wa kiuchumi ili kulinda mfumo wa kimataifa. Baerbock amesisitiza kuwa idadi kubwa ya nchi bado zimejitolea kwa mfumo wa ushirikiano wa kimataifa, “Nchi 193 ukiondoa chache bado zinawakilisha wingi mkubwa.”