Dar es Salaam. Familia ya raia wa Israel, Inbar Greidinger-Geisler, aliyepoteza maisha kwa ajali akifanya utalii katika Hifadhi ya Ngorongoro, imeiandikia barua Mahakama ya Wilaya ya Ngorongoro ikiilalamikia kutomchukulia hatua mshtakiwa wa kesi ya ajali hiyo.

Wameeleza kuwa mshitakiwa anachelewesha kesi hiyo kutokana na kutofika mahakamani mara kadhaa na kuiomba ichukue hatua stahiki dhidi yake.

Ajali hiyo ilitokea Januari 4, 2025, katika eneo la Kona ya Sukari, ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro, Wilaya ya Ngorongoro, Mkoa wa Arusha, wakati gari walilokuwa wakisafiria wanafamilia hao lilipopinduka.

Katika ajali hiyo mwanafamilia mmoja Inbar, mwanamke mwenye umri wa miaka 29, alipoteza uhai huku wanafamilia wengine watano wakijeruhiwa.

Kutokana na ajali hiyo dereva aliyekuwa akiliendesha gari hilo aina ya Toyota Land Cruizer, Tumaini Mkonyi pamoja na mmiliki gari hilo, Charles Melikior Mullo walipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Ngorongoro kwa nyakati tofauti.

Kila mmoja alisomewa mashtaka yake kwa wakati wake, lakini wote wakidaiwa kuyatenda Januari 4, 2025, katika Kona ya Sukari, ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro, wilayani Ngorongoro, mkoani Arusha.

Dereva Tumaini aliposomewa mashtaka yake ya kuendesha kwa uzembe na kusababisha kifo, majeraha, kuendesha gari bila leseni na kuharibu gari alikiri kutenda makosa hayo akatiwa hatiani na kuhukumiwa adhabu ya kulipa faini ya Sh120,000.

Hata hivyo, mmiliki wa gari hilo, Mullo alikana kosa lake la kumruhusu mtu kuendesha gari lake bila kuwa na faini na akaachiwa kwa dhamana, lakini anadaiwa kuwa amekuwa hafiki mahakamani mara kadhaa na kusababisha kesi kukwama.

Kutokana na mwenendo huo Desemba Mosi, 2025 familia hiyo ya marehemu kupitia kwa wakili wake kutoka Ernestilla Mafita & Co. Advocates, waliiandikia mahakama hiyo barua ya malalamiko dhidi mwenendo huo wa mshtakiwa, huku ikimkalia kimya bila kumchukulia hatua.

“Tunawasilisha rasmi malalamiko haya kuhusu ukiukwaji wa mara kwa mara wa masharti ya dhamana unaofanywa na mshtakiwa wa pili, Charles  Mullo,” inasomeka barua hiyo mwanzoni kabisa, ambayo Mwananchi imeona nakala yake, iliyosainiwa na Ernestilla John, mshirika mkuu wa kampuni hiyo.

Barua hiyo imeelekezwa kwa Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo, imewasilishwa mahakamani hapo katika mfumo wa mahakama wa usajili wa mashauri na uwasilishaji wa nyaraka mbalimbali za kesi kwa njia ya kielektroniki, imesajiliwa katika mfumo huo Desemba 3, 2025.

Ikifafanua malalamiko hayo barua hiyo inaeleza kuwa mshtakiwa huyo aliyeko nje kwa dhamana anatakiwa kuhudhuria mahakamani kila tarehe iliyopangwa, kama inavyoelekezwa katika kifungu cha 151(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA), Sura ya 20, Toleo la 2023.

“Pamoja na wajibu huo wa kisheria, kwa heshima tunafahamisha Mahakama hii tukufu ukweli kwamba mshtakiwa wa pili alishindwa kufika mahakamani katika kikao kilichopita (Novemba 20,  2025) na Desemba Mosi, 2025,” inaeleza barua hiyo na kusisitiza:

“Kutokuwepo kwake hakukuambatana na sababu yoyote ya msingi, wala hakukuwa na nyaraka za kitabibu kuthibitisha madai ya ugonjwa yaliyowasilishwa kupitia kwa mdhamini wake.”

Inaeleza licha ya ukiukwaji huo wa wazi wa masharti ya dhamana, shauri hilo liliahirishwa hadi Januari 2, 2026, tarehe ambayo ilizidi kikomo cha kisheria cha siku 14 cha kuahirisha shauri la jinai.

Mawakili hao wanaeleza katika barua hiyo ucheleweshaji huo wa shauri hilo unakwamisha bila sababu utekelezaji wa haki katika shauri ambalo tayari limesababisha maumivu makubwa kwa familia ya marehemu.

Wamesema familia hiyo inatoa shukurani za dhati kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa msaada mkubwa uliotolewa ikiwemo, kwa ombi la Rais wa Israel, kusaidia familia katika taratibu zote muhimu za kuurudisha mwili wa mpendwa wao nyumbani.

Hata hivyo, wameeleza inashindwa kuelewa ni kwa namna gani mtu aliyewajibika kwa kuajiri dereva asiye na leseni, kitendo kilichosababisha kukatizwa ghafla kwa maisha ya binti yao mwenye matumaini makubwa, anaweza kuruhusiwa kukosa kuhudhuria mahakamani bila kuchukuliwa hatua madhubuti.

Wameeleza kutokana na mazingira hayo, wana wasiwasi mkubwa juu ya kusita kwa Mahakama kutoa hati ya kukamatwa na kwamba hali hiyo inatoa taswira ya kutia shaka kwamba mshtakiwa wa pili anatendewa kana kwamba yuko juu ya sheria.

Mawakili hao wanasisitiza kwamba kuendelea kuahirisha shauri hilo kunakiuka haki ya familia ya marehemu ya kupata haki kwa wakati.

Hivyo wameiomba mahakama hiyo ichukue hatua stahiki kwa mshtakiwa huyo kutokana na mwenendo wake huo wa ukiukaji wa masharti ya dhamana.

Hatua hizo wanazozipendeleza ni pamoja na kufuta au kurekebisha masharti ya dhamana, kutoa maelekezo madhubuti ili kuhakikisha shauri linaendelea bila ucheleweshaji zaidi, kwa mujibu wa matakwa ya kisheria.

Mbali na hatua hizo walizopendekeza pia wameiomba mahakama hiyo kutoa amri nyingine zozote zitakazohakikisha kuhudhuria kwa mshtakiwa, na hivyo kulinda haki ya waathirika na familia yao ya kupata haki kwa wakati na kwa ufanisi.

Kwa mujibu wa mwenendo wa kesi hiyo ambao Mwananchi limeuona, mara ya mwisho ilitajwa Januari 2, 2026, na ingawa hakimu anayeisikiliza, Hakimu Mkazi Mkuu, Bethsaida Sivonike hakuwepo, lakini siku hiyo pia mshtakiwa Mullo hakufika mahakamani.

Hivyo kesi hiyo iliahirishwa mpaka keshokutwa Ijumaa, Januari 23, 2026.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *