Kauli ya UNESCO imo kwenye taarifa iliyochapishwa kwenye wavuti wa shirika hilo ikisema serikali badala yake zinapaswa kuhakikisha kuwa raia wanatekeleza haki zao za kidemokrasia, hasa zaidi nyakati za migogoro, kupitia matumizi ya mtandao na majukwaa mengine ya mtandaoni.

Mwaka 2024 ulivunja rekodi ya matukio ya serikali kuzima intaneti

Ikinukuu taasisi ya Access Now, UNESCO imesema matukio 300 ya kuzimwa kwa mtandao yameripotiwa katika zaidi ya nchi 54 ndani ya kipindi cha miaka miwili iliyopita; ambapo mwaka 2024 ulikuwa mwaka wenye matukio mengi zaidi kuwahi kushuhudiwa tangu 2016.

“Tangu mwanzo wa mwaka huu wa 2026, kuzimwa kwa mtandao kwa nchi nzima kumefanyika katika nchi zinazokumbwa na maandamano makubwa au zilizo katikati ya michakato ya uchaguzi,” imesema taarifa hiyo.

UNESCO imekuwa ikionya mara kwa mara dhidi ya usumbufu wa watu kukatiwa mtandao na “serikali zitekeleze sera zinazorahisisha upatikanaji badala ya kuweka vikwazo vya muunganisho.”

Kupata taarifa kwa wakati ni haki ya msingi

Shirika hilo linakumbusha kuwa upatikanaji wa taarifa ni sehemu muhimu ya haki ya msingi ya uhuru wa kujieleza, na ni nguzo kuu katika utekelezaji wa haki mbalimbali za binadamu, zikiwemo haki ya elimu, uhuru wa kujumuika na kukusanyika, na ushiriki katika maisha ya kijamii, kitamaduni na kisiasa.

“Kuzimwa kwa mtandao hakuleti madhara kwa waandishi wa habari pekee, wafanyakazi wa vyombo vya habari na shughuli za utoaji wa taarifa na habari zilizothibitishwa, bali pia unaleta madhara kwa kiasi kikubwa kwenye upatikanaji wa taarifa za umma kwa wananchi,” imesema UNESCO.

Na kama hiyo haitoshi, UNESCO inasema kuwa “kuvurugwa kwa mnyonyoro huu muhimu hakudhoofishi tu uadilifu wa taarifa, bali pia husababisha kuenea kwa taarifa zisizothibitishwa na zinazoweza kuwa hatarishi,” kama ambavyo UNESCO imeeleza mara kadhaa, kuanzia maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Upatikanaji wa Taarifa kwa Wote  mwaka 2023, hadi Jukwaa la Kisiasa la Ngazi ya Juu la mwaka 2024, pamoja na Miongozo ya UNESCO kuhusu Uendeshaji wa Majukwaa ya Kidijitali.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *