Ili kupata majaji na mahakimu watenda haki, ni muhimu Tanzania ikaachana na mfumo wa uteuzi wa hisani na badala yake ijenge utaratibu wa wazi, shirikishi na wa ushindani unaohusisha kuomba kazi, kufanya usaili na kuteua wenye uwezo pekee.

Pendekezo hili linahusu nafasi zote za kimahakama, kuanzia mahakimu, majaji hadi Jaji Mkuu wa Tanzania.

Ninaanza kwa kutangaza maslahi yangu. Pamoja na kuwa mwandishi wa habari na mtangazaji wa kujitegemea, mimi pia ni mwanasheria na wakili wa kujitegemea ninayejihusisha na kutoa elimu kwa umma kuhusu Katiba, sheria, haki na wajibu.

Kwa kuwa kila wakili ni ofisa wa mahakama na kwa kutambua heshima kubwa wanayopewa majaji, ushauri wa kutaka majaji waombe kazi haupaswi kutafasiriwa kama dharau.

Lengo ni kuboresha mfumo wa utoaji haki, si kupunguza heshima ya mhimili wa Mahakama.

Kwa muda mrefu changamoto ya ukosefu wa haki katika Mahakama imekuwa ikijitokeza, ikichangiwa na uwepo wa baadhi ya mahakimu na majaji wenye uwezo mdogo wa kubaini haki. Katika mazingira hayo, watuhumiwa hubambikiwa kesi au ushahidi wa uongo, huku mhusika anayesimamia kesi akishindwa kutambua dosari hizo.

Matokeo yake ni watu wasio na hatia kuhukumiwa vifungo vya jela kwa makosa wasiyoyatenda, jambo ambalo ni dhulma, ni kinyume cha haki za binadamu na ni kosa la kimaadili.

Athari za hukumu za kubambikiza hazimuathiri mtuhumiwa pekee. Familia, ndugu na jamaa huingia katika mateso makubwa ya kisaikolojia, kiuchumi na kijamii.

Wapo wanaorejea kutoka gerezani na kukuta familia zao zimesambaratika, watoto wameacha shule na mahusiano kuvunjika.

Hali hii kwa kiasi kikubwa inatokana na mfumo wa uteuzi unaotegemea kuteua bila mchakato wa ushindani.

Mahakimu na majaji wenye uwezo wa kweli huwa na kile kinachoweza kuitwa jicho la haki, uwezo wa ndani wa kutambua dhulma hata kabla ya ushahidi wa kina.

Wanapomsikiliza mtuhumiwa na mashahidi, huweza kubaini kama kesi ni ya kubambikiwa au la, na kufanya uamuzi wa haki kwa ujasiri.

Mfano wa kesi zinazoibua mjadala huu unaonekana katika matukio ya hivi karibuni ambapo baadhi ya raia, wakiwemo vijana, wamekumbwa na mashtaka mazito yanayotajwa kuwa ya kubambikiza.

Katika muktadha huo, Watanzania wanapaswa kutambua hatua zilizochukuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kuelekeza kufutwa kwa baadhi ya kesi zisizo na ushahidi wa kutosha.

Ili kuondoa tatizo hili kwa msingi wake, kunahitajika mabadiliko ya mfumo. Nafasi zote za mahakama zinapaswa kutangazwa wazi. Watanzania wenye sifa waombe kazi, wafanyiwe usaili wa wazi na wa ushindani, na wateuliwe kwa kuzingatia uwezo, maadili na uadilifu.

Katika usaili huo, kuwepo na vipimo maalum vya kutathmini uwezo wa mhusika kubaini haki na kufanya maamuzi yenye mizani ya haki.

Kwa sasa, utaratibu uliopo ni majaji kupendekezwa na Tume ya Utumishi wa Mahakama na majina kupelekwa kwa Rais kwa uteuzi, bila waombaji kuomba wala kusailiwa. Utaratibu huu ulifaa wakati idadi ya wanasheria wenye sifa ilikuwa ndogo.

Hata hivyo, Tanzania ya sasa ina wanasheria wengi wenye vigezo vya ujaji, hivyo hakuna sababu ya kuendelea na mfumo usio shindani.

Nchi jirani ya Kenya imeonesha mfano mzuri, ambapo hata Jaji Mkuu huomba kazi na kusailiwa hadharani. Mfumo huo umeongeza uwazi, uwajibikaji na imani ya wananchi kwa Mahakama.

Hoja hii inapata uzito zaidi kufuatia kauli ya Rais Samia alipokuwa akifungua Mkutano Mkuu wa Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMA) mkoani Dodoma, ambapo alikiri kuwepo kwa wafungwa walioko gerezani kwa kesi za kubambikiwa.

Alisisitiza umuhimu wa kuharakisha upelelezi, kuachia huru wanaoshikiliwa bila ushahidi wa kutosha na kulinda uhuru wa Mahakama.

Mahakama ni mhimili wa msingi wa Taifa linalozingatia utawala wa sheria.

Ili iendelee kuaminika, lazima iendeshwe na majaji na mahakimu waliopitia mchakato wa wazi, wa haki na wa ushindani, ili haki ionekane na itendeke.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *