Dar es Salaam. Uhusiano wa Harmonize na Kajala Masanja umekuwa na matukio mengi ya panda shuka ambayo kwa miaka zaidi ya minne sasa yamekuwa yakigonga vichwa vya habari na kuvutia usikivu wa mashabiki.
Sasa kwa kulitambua hilo, tunakuletea mtiririko wa matukio ya urafiki hadi uhusiano wao tangu walipoanzana, kuachana, kurudiana na hadi sasa ambapo wamerudiana kwa mara nyingine tena.
Agosti 2017: Harmonize anamtaja Kajala
Katika wimbo wa WCB Wasafi, Zilipendwa (2017), ndipo Harmonize alimtaja Kajala kwa mara ya kwanza ila haikujadiliwa, wakati huo uhusiano wao ulikuwa haujulikani ila hatuwezi kusema ilikuwa bahati mbaya.
“P-Funk Kajala (zililipendwa). Onyango na Jangala (zilipendwa),” aliimba Harmonize katika wimbo huo uliokutanisha wasanii wengine kama Diamond Platnumz, Rich Mavoko, LavaLava, Queen Darleen, Rayvanny na Mbosso.
Kwa mujibu wa mahojiano mapya ya Kajala, uhusiano wao ulianza kitambo – wakati Paula akiwa sekondari na aliwahi kumlipia ada akiwa kidato cha pili, hivyo huenda Harmonize alimaanisha jambo katika wimbo huo.
Februari 2021: Wanathibisha kuwa pamoja
Baada ya tetesi za muda mrefu huku wakiteka mazungumzo katika mitandao ya kijamii, hatimaye Februari 2021, Harmonize na Kajala waliweka hadharani uhusiano wao wakionekana pamoja katika matukio kadhaa.
Hatua hiyo ilikuja siku chache baada ya Harmonize kusitisha ziara yake kimuziki (In The Club Tour) kwa madai kuwa hali yake ya kiafya sio nzuri. Ziara hiyo ilianzia Mwanza na ilipangwa kupita mikoa mingi nchini.
Kusitishwa kwa ziara hiyo kukatoa fursa kwa uhusiano wao kukua mbele ya macho ya umma huku kukiwa na mjadala uliojikita katika tofauti ya umri wao (takribani miaka 10), mjadala ambao kwa sasa hausikiki tena.
Februari 2021: Ugomvi mzito unaibuka
Wakati uhusiano ukiendelea kupamba moto, ghafla linatokea tukio la aibu. Ni video za Harmonize zinazodaiwa alikuwa akimshawishi binti wa Kajala, Paula ili kuwa naye kimapenzi ilihali yupo na mama yake!
Ni sakata lililowafikisha wote polisi akiwamo Rayvanny ambaye wakati huo alikuwa na Paula, uhusiano ambao ulikuja kuisha kwa ugomvi huku Kajala akitupa lawama kwa Hamisa Mobetto akidai ndiye aliwakutanisha.
Hata hivyo, katika mfululizo wa vipindi vyao, Behind The Gram, Paula alikiri kwa kinywa chake akidai kuwa anamchukia Harmonize kwa sababu alimtongoza wakati anajua bado ana uhusiano na Kajala (mama yake).
Novemba 2021: Harmonize ana-move on!
Akiwa anaendelea na ziara yake ya muziki nchini Marekani hapo Novemba 2021, Harmonize akamtambulisha Briana kutokea Australia kama mpenzi wake mpya, na baada ya ziara hiyo alikuja naye Bongo.
Hata hivyo, uhusiano huu ulidumu kwa muda wa miezi mitano tu, hivyo waliachana Machi 2022, ukiwa ni uhusiano wa nne wa Harmonize uliowekwa hadharani kuvunjika.
Ikumbukwe tayari alikuwa ameshaachana na Kajala, Jacqueline Wolper na Sarah kutokea Italia ambaye walifunga hadi ndoa ila nayo ilivunjika kwa madai ya usaliti baada ya kudumu kwa takribani mwaka mmoja.
Aprili 2022: Harmonize anamlilia Kajala
Baada ya kuachana na Briana, Harmonize alianza kutuma mfululizo wa jumbe kupitia Insta Story akieleza kuwa anahitaji kurudiana na Kajala, huku wapambe wake mbambali nao wakimsaidia suala hilo.
Harmonize alieleza kuwa watu wanaweza kumuona mwenye furaha lakini sivyo, anachotaka ni familia yake kurejea nyumbani. Familia hiyo ni Kajala na binti yake, Paula ambao alikuwa akiishi nao hapo awali.
Hatua hiyo ilikuja baada ya Harmonize kutoa wimbo, Mtaje (2021) ambao ulikuwa maalum kwa ajili ya kumbembeleza Kajala. Moja ya mistari yake inasema; “mwambieni mwanangu Paula mimi nampenda mamaye.”
Juni 2022: Kajala anavishwa pete
Harmonize alifanikiwa kumshawishi Kajala arejee kwake, jambo ambalo wengi hawakutegemea kutokana na yale yalitokea kati yao lakini hayo ndio mapenzi, muda mwingine yanaonyesha maajabu yake.
Awamu hii Harmonize alikuja kiutofauti kidogo akionyesha kuwa amedhamiria kufanya kitu, ndipo akachukua hatua ya kumvisha Kajala pete ya uchumba, hatua ambayo ilimtoa machozi mrembo huyo.
Tukio hilo ambalo lilifanyika Juni 25, 2022 katika hoteli ya Serena, Dar es Salaam, Paula naye alihudhuria, na huu ulikuwa ni uthibitisho kuwa amesamehe yote aliyodai kutendewa na yupo tayari kwa ukurasa mpya ujao.
Septemba 2022: Kajala katika video
Kwa mara ya kwanza Kajala anatokea katika video ya Harmonize, nayo ni ya wimbo, Nitaubeba (2022), katika video hiyo walivalia kama bwana na bibi harusi wenye furaha kubwa baada ya kufunga ndoa.
Katika wimbo huu, Harmonize anamwambia mke wake kuwa kabla ya kulala, humuomba Mungu amlinde na kumtunza, kwa sababu yeye ni pacha wake wa maisha.
Anaeleza kuwa atakuwa naye bega kwa bega katika nyakati zote – wakati wa shida na tabu, furaha na huzuni, shibe na njaa. Wimbo huu unaakisi upendo wa dhati, uaminifu na mshikamano wa kweli katika ndoa.
Desemba 2022: Wanaachana tena!
Takribani miezi sita tangu kuchumbiana, wawili hao waliachana ikiwa ni mara ya pili, huku kukiwa na madai kuwa Kajala alichukua gari (Range Rover) alilozawadiwa na kwenda kulificha akihofia kupokonywa.
“Nimeikosea sana familia yangu, ndugu zangu na marafiki. Kufanya kosa sio kosa ila kurudia kosa ndio makosa makubwa. Ninamsamehe ex wangu na niko tayari kwa mwingine,” alieleza Kajala.
Hata hivyo, mara zote ambazo wamekuwa wakiachana, Kajala hajawahi kumuweka hadharani mtu ambaye yupo naye kwa wakati huo zaidi ya kusema ana mtu mwingine, kitu ambacho ni tofauti kwa Harmonize.
Februari 2023: Anafuta tattoo ya Kajala, Paula!
Mwezi mmoja baada ya kuachana kwao, inaaminika kuwa Harmonize alichukua uamuzi wa kufuta tattoo ya Kajala na Paula ambayo alikuwa ameichora katika mguu yake.
Katika video iliyoiposti Instagram akiimba na kucheza wimbo wake, Single Again (2023), tattoo ilionekana imefutwa lakini haikujulikana ni lini hasa aliamua kuchukua uamuzi huo.
Awali, mapema mwezi huo akiwa Kenya aliulizwa kwanini bado hajaifuta tattoo hiyo, na jibu la Harmonize lilikuwa – Tattoo ni suala binafsi, sidhani kama naweza kuzungumzia. Tuangalie tu kama itaendelea kuwepo.
Mei 2023: Paula anaumizwa na Harmonize
Kwa mujibu wa Kajala, binti yake, Paula aliwahi kumueleza kuwa madai ya kuambiwa ame-share mwanaume (Harmonize) na mama yake mzazi yalimuumiza sana na ni kitu kitakachomtafuna katika maisha yake yote.
“Paula anaweza kuwa amesema nimekusamehe kwa sababu mimi ni mama yake ananipenda, lakini sijui moyo yuko vipi,” alisema Kajala kwenye Behind The Gram na kuongeza:
“Kuna siku ashawahi kunitamkia akaniambia, ‘Unadhani mimi watoto wenzangu wananichukulia vipi kwamba mimi nime-share mwanaume na mama yangu?’, akaendelea kusema ‘hii itanila maisha yangu yote’,” alisema.
Julai 2023: Kajala anajutia tattoo
Akizungumza katika show yake na Paula, Behind The Gram, Kajala alisema anajutia kuchora tattoo yenye jina la Harmonize mwilini mwake na ana mapango wa kuifuta huku akisisitiza kutorudia kufanya hivyo.
“Inabidi nifute na hii tattoo, niliichora katika mapenzi, ni mtu ambaye nilikuwa nampenda. Kwanza katika maisha sitakuja kumchora mtu, mpenzi au boyfriend tattoo,” alisema Kajala.
Ikumbukwe Kajala katika shingo yake nyuma sikio kidogo ndipo alichora tattoo hiyo ikiwa na neno “H” akimaanisha Harmonize ambaye naye alifanya kitu kama hicho akichora neno “K”, yaani Kajala.
Agosti 2023: Harmonize anatoa siri
Baada ya Harmonize kutopendezwa na kauli fulani aliyoitoa Kajala kumhusu, aliamua kwenda Insta Story na kueleza mambo mengi aliyomsaidia Kajala hadi ya kifamilia ila mwisho wa siku amekosa shukrani kwake.
Harmonize alidai aliona yeye anamiliki magari zaidi ya 10, lakini mpenzi wake [Kajala] hana hata moja, hivyo akaamua kumpa gari akimmilikisha kihalali kabisa, lakini bado anaonekana mbaya!
Alienda mbali zaidi akisema hata simu anayotumia Kajala kwa kumzungumzia vibaya mtandaoni yeye ndiye aliinunua, na pia amewahi kutoa misaada mingi sana nyumbani kwao ikiwamo kusaidia ujenzi wa ukuta.
Januari 2024: Harmonize, Poshy Queen penzini
Mapema Januari 2024, Poshy Queen aliposti video Instagram akiwa kwenye mbuga za wanyama, katika moja ya video ilisikika sauti ya Harmonize na ndipo zikaanza tetesi kuwa wawili hao wana uhusiano.
Baada ya muda, Poshy Queen aliposti picha ya Harmonize Instagram na kuandika; Adam wangu mimi hapa. Harmonize alijibu ujumbe huo akieleza kuwa tangu mwaka 2017 wapo pamoja!.
“Sio tu damu hata figo nakutolea Eva, tangu 2017, sasa tumefika hapa. Ni historia kubwa ya kusimulia kwa Nova na Zuuh Konde – wanapaswa kuwa na subira,” alieleza Harmonize ila walikuja kuachana Agosti 2024.
Mei 2025: Harmonize, Kajala wanakutana tena!
Katika sherehe ya kumbukizi ya kuzaliwa mtoto wa Paula na Marioo, Harmonize alihudhuria na muda mwingi alionekana kuwa karibu na Kajala hata ilifikia wakati wakacheza muziki pamoja.
Hiyo ilitoa picha kuwa wamerudiana, siku iliyofuatia, Harmonize alirejesha picha za Kajala katika ukurasa wake wa Instagram ambazo alikuwa amezificha, lakini baada ya muda akaziondoa tena.
Mbali na Kajala, Harmonize alihudhuria shughuli hiyo kutokana na ukaribu ulionao na Marioo ambaye wameshirikiana katika nyimbo nyingi – Naogopa (2022), Away (2024), Disconnect (2024), Wangu (2024) n.k.
Desemba 2025: Kajala anavishwa pete tena!
Siku moja baada ya Kajala kutokea katika show ya Harmonize iliyofanyika Zanzibar, staa huyo alidokeza kuwa yupo tayari kumvisha pete Kajala tena.
“Katika jina langu kuna jina lako, na katika jina lako kuna jina langu. Dunia nzima inafurahia kwa ajili yetu. Endapo mkono wako utapokea, nitaweka pete kwenye kidole chako tena. Tuanze upya,” alieleza.
Desemba 29, 2025, ndani ya boti akamvisha tena!
Miongoni mwa walioshuhudia ni Paula. Je, mwaka 2026 utakuwaje kwa wawili hao? Tungoje.