Dar es Salaam. Yanga imetamba kuwa haina mpango wa kujilinda katika mchezo wake wa ugenini wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly, jijini Alexandria, Misri, Ijumaa wiki hii.

Wawakilishi hao wa Tanzania, wamejinadi kwamba lengo la kwanza ni kupata ushindi katika mechi hiyo na ikiwa kinyume ni sare lakini sio kupoteza mechi.

Mchezo huo utachezwa katika Uwanja wa Borg El Arab, Ijumaa kuanzia saa 1:00 usiku kwa muda wa Afrika Mashariki.

Akizungumza wakati msafara wa timu hiyo unaondoka jana alfajiri kuelekea Misri, Kocha Mkuu wa Yanga, Pedro Goncalves amesema kuwa usajili walioufanya kwenye dirisha dogo umewapa kikosi ambacho kinawapa imani kwamba wanaweza kupambana na klabu yoyote barani Afrika.

Pedro amesema kuwa wamepata wachezaji ambao wametengeneza timu yenye uwiano sahihi kutokana na ubora wa nyota walioingia wakiungana na wale ambao walikuwepo hivyo licha ya ukubwa, ubora na historia ya Al Ahly, Yanga haina sababu ya kucheza kwa mbinu ya kuzuia na badala yake itashambulia kwa muda mwingi wa mchezo.

“Tupo tayari kukutana na Al Ahly. Ni timu ngumu na yenye rekodi kubwa Afrika. Tutawafuata tukijua taarifa zao lakini jambo zuri ni kwamba tuna timu imara. Tumefanya usajili ambao umetufanya kuwa na kikosi kilichokuwa na uwiano mzuri.

“Nina furaha na ubora wa wachezaji wangu na tutakwenda  kutumia ubora wa kikosi chetu kutafuta matokeo ya aina mbili tu kushinda au kutoa sare. Haitakuwa mechi rahisi lakini hatuwezi kuwa timu ambayo itasubiri wapinzani wetu kuamua mchezo,” alisema Pedro.

Katika dirisha dogo la usajili linaloendelea, Yanga imewanasa kipa Hussein Masalanga viungo Mohammed Damaro na Allan Okello pamoja na washambuliaji Emmanuel Mwanengo na  Laurindo  Aurélio ‘Depu’ huku ikiwatoa watatu kwa mkopo ambao ni Denis Nkane, Selestin Ecua na Mamadou Doumbia huku Andy Boyeli aliyekuwa anacheza kwa mkopo akirudishwa timu yake ya Sekhukhune ya Afrika Kusini.

Pedro alisema ujio wa wachezaji wapya na wale waliokuwepo umeongeza ushindani mkubwa ambapo kila mchezaji ameongeza hamasa ya kupigania nafasi jambo ambalo anaamimi litawachochea kufanya vizuri.

“Ukiangalia kuanzia mazoezini kuna ari kubwa imeongezeka ya kupigania nafasi, kila mchezaji anajituma zaidi kwa sasa. Hatua kama hii itatupa nafasi ya kufanya maamuzi mazuri ya nani aanze au nani acheze mechi ipi.

“Tuna timu pana ambayo sasa tunaweza kuchagua mifumo bora zaidi lakini kutoa nafasi kwa kila mchezaji kucheza. Kama nilivyokwambia tuna mechi nyingi katika mashindano tofauti, lazima tuwe na hesabu za kuwapumzisha wachezaji,” alisema Pedro.

Ushindi katika mchezo dhidi ya Al Ahly utaifanya Yanga iongoze msimamo wa kundi B ambapo itafikisha jumla ya pointi saba.

Kwa sasa kinara wa kundi hilo ni Al Ahly ambayo ina pointi sawa na Yanga zote zikiwa na pointi nne kila moja, lakini timu hiyo yan Misri inabebwa na utofauti mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa ambapo imepachika matano na kuruhusu mawili huku Yanga ikifunga moja bila kuruhusu nyavu zake kutikiswa.

Timu nyingine kwenye kundi hilo ni FAR Rabat ya Morocco na JS Kabylie ya Algeria zenye pointi moja kila timu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *