Dakar, Senegal. Rais wa Senegal, Bassirou Faye ametoa zawadi ya Dola 135,000 (Sh342 milioni) pamoja na kipande cha ardhi chenye ukubwa wa mita za mraba 1,500 katika eneo la Petite Côte, Senegal kwa kila mchezaji wa timu ya taifa hilo aliyekuwemo katika kikosi kilichotwaa Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 Jumapili iliyopita huko Morocco.

Senegal ilitwaa ubingwa huo kwa kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya wenyeji Morocco.

Mbali na zawadi hizo, Rais Faye pia amemtunuku Kocha Mkuu wa timu, Pape Thiaw pamoja na wachezaji kwa kuwapa hadhi ya ‘Commander of the National Order of the Lion’, heshima ya juu ya kitaifa inayotolewa kwa watu waliotoa mchango mkubwa kwa taifa lao.

Akizungumza katika hafla ya utoaji wa tuzo hizo, Rais Faye amesema ubingwa wa AFCON 2025 umeiletea Senegal heshima kubwa barani Afrika na duniani kwa ujumla, akibainisha kuwa mafanikio hayo yameimarisha mshikamano wa kitaifa.

Ameongeza kuwa kocha na wachezaji wamekuwa mabalozi wazuri wa nchi kupitia michezo, wakionesha nidhamu, mshikamano na uzalendo wa hali ya juu.

“Walifanya kwa ushujaa, walicheza soka la kuvutia, walikuwa waungwana kupita kiasi na walikuwa mfano wa kuigwa uwanjani na nje ya uwanja. Tunaweza tu kujivunia wao,” alisema Rais Faye.

Katika fainali dhidi ya Morocco, bao pekee la Pape Gueye katika dakika ya 94 ya mechi hiyo iliyochezwa kwa dakika 120, lilitosha kuipa ushindi Senegal dhidi ya wenyeji, katika mechi ambayo iliyogubikwa na matukio ya vurugu na mgomo.

Penalti ambayo Morocco waliipata katika dakika za lala salama kabla ya dakika 90 kumalizika, ilimfanya Kocha Thiaw kuamrisha wachezaji wake kutoka nje ya uwanja ikiwa ni ishara ya kutokuwa tayari kuendelea na mchezo.

Hata hivyo, baadaye walirejea uwanjani kuendelea na mchezo ndipo Brahim Diaz wa Morocco alikosa mkwaju wake wa penalti uliookolewa na kipa wa Senegal, Edouard Mendy.

Dakika 30 za nyongeza za mechi hiyo zilionekana kuwa na neema kwa Senegal ambayo ilipata bao pekee kupitia kwa Gueye ambalo lilihakikishia taji hilo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *