Katika kipindi cha hivi karibuni, kumekuwa na ongezeko la malalamiko kutoka kwa wananchi wanaopoteza fedha zao kupitia utapeli wa kimtandao unaohusisha simu za mkononi.

Kinachotia wasiwasi zaidi ni kwamba visa hivi havitokei kwa nguvu au vitisho vya silaha, bali kwa hila, udanganyifu na matumizi mabaya ya teknolojia. Hili linaonesha kwamba kadri huduma za fedha za kidijitali zinavyozidi kukua, ndivyo umuhimu wa usalama wake unavyopaswa kupewa kipaumbele.

Hakuna shaka kwamba maendeleo ya sayansi na teknolojia yameleta mapinduzi makubwa katika maisha ya watu. Huduma ambazo hapo awali zilihitaji uwepo wa mtu katika ofisi au tawi la taasisi, leo zinapatikana kwa urahisi kupitia simu ya mkononi.

Sekta ya fedha ni miongoni mwa sekta zilizonufaika kwa kiwango kikubwa zaidi na mabadiliko haya. Kupitia huduma za fedha kidijitali, mamilioni ya wananchi sasa wanaweza kuhifadhi, kutuma, kupokea, kufanya malipo na hata kukopa fedha kwa urahisi na kwa gharama nafuu.

Hata hivyo, pamoja na mafanikio haya, ukuaji wa huduma za fedha kidijitali umeibua changamoto mpya – usalama. Mathalani katika robo ya tatu ya mwaka 2025, takwimu za TCRA zilionyesha kuwa kulikuwa na majaribio ya ulaghai wa kimtandao yapatayo 12,475 asilimia kubwa yakifanyika katika mikoa ya Rukwa, Morogoro na Dar es Salaam.

Kama kiongozi wa moja ya taasisi zinazotoa huduma za fedha kidijitali nchini, natambua kikamilifu wajibu mkubwa tulionao wa kulinda fedha na taarifa za wateja wetu kwa viwango vya juu kabisa vya usalama, na nina dhamira thabiti pamoja na umakini mkubwa katika kuhakikisha usalama wa fedha za wateja wetu.

Watoa huduma wengi wamekuwa wakiboresha mifumo yao mara kwa mara ili kukabiliana na vitisho vinavyoibuka kila siku. Maboresho haya yanajumuisha matumizi ya teknolojia za kisasa, ufuatiliaji wa miamala kwa wakati halisi, pamoja na kuweka mifumo madhubuti ya udhibiti wa hatari. Hatua hizi si za hiari, bali ni za lazima katika mazingira ya sasa ya kidijitali.

Kwa mfano, hapa Mixx, tumechukua hatua mahususi za kuimarisha usalama kwa kuwapa wateja uwezo wa kuidhinisha miamala kupitia teknolojia za kibayometriki zinazopatikana katika aplikesheni yetu ya Mixx Super App, teknolojia hii inahakikisha kuwa ni mmiliki halali wa akaunti pekee anayeweza kuruhusu muamala kufanyika, hivyo kupunguza kwa kiasi kikubwa hatari ya matumizi yasiyoidhinishwa.

Aidha, tunafanya ukaguzi wa mara kwa mara wa mifumo na taratibu zetu kwa kushirikiana na wakaguzi wa ndani na wa nje. Ukaguzi huu hutusaidia kubaini mapungufu, kuimarisha mifumo ya udhibiti, na kuhakikisha kuwa tunazingatia viwango vya kitaifa na kimataifa vya usalama wa huduma za fedha kidijitali. Jitihada hizi zimeiwezesha huduma yetu kupata vyeti vya kimataifa vinavyothibitisha kuwa fedha na taarifa za wateja zinalindwa kwa kiwango cha juu muda wote.

Jitihada hizi ndizo zimeiwezesha Mixx kupata cheti cha kimataifa cha GSMA Mobile Money Certification, ambacho kinathibitisha kuwa fedha na taarifa za wateja zinalindwa na kuhifadhiwa kwa usalama wa hali ya juu muda wote.

Hata hivyo, ni muhimu kusisitiza kuwa usalama wa fedha kidijitali hauwezi kupatikana kwa juhudi za watoa huduma pekee. Ushiriki wa mtumiaji ni nguzo muhimu katika mnyororo wa usalama. Uzoefu unaonesha kuwa visa vingi vya utapeli vina dalili zinazofanana ambazo mtumiaji anaweza kuzitambua mapema iwapo atakuwa makini.

Dalili za kwanza ni kupokea simu inayomtaka mtumiaji kutoa taarifa binafsi huku namba ya mpiga simu siyo namba rasmi ya huduma kwa wateja, kama vile namba 100 ambayo ndiyo pekee inayotumiwa na mitandao ya simu kuwasiliana na wateja wake as approved by regulators.

Dalili ya pili ni ujumbe mfupi unaomtaka mtumiaji kubofya kiunganishi (link) au kutimiza masharti fulani ambayo hayatoki kwa mtoa huduma husika au kutuma hela Kwenda namba nyingine.

Dalili ya tatu ni shinikizo la haraka wahusika wanataka mtumiaji achukue hatua mara moja kama kutoa taarifa zake binafsi kuepuka kukosa huduma au kutuma hela kana kwamba kuna dharura au kutuma hela kama vile mtoto kuwa hospitalini au ajali, mara nyingi wakitumia vitisho au maneno ya kutisha.

Dalili ya nne, na iliyo hatari zaidi, ni kuombwa taarifa nyeti kama PIN au nenosiri, salio la akaunti , namba za kitambulisho, au namba za uthibitisho (OTP), ambazo kamwe hazipaswi kutolewa kwa mtu mwingine yeyote.

Ni kweli usalama wa fedha kidijitali ni wajibu wa pamoja; unahitaji mifumo imara na salama kutoka kwa watoa huduma, usimamizi makini kutoka kwa wadhibiti wa sekta, na nidhamu ya kila mtumiaji katika kulinda taarifa zake binafsi.

Tushirikiane kulinda fedha zako kwani usalama wa fedha zako ni dhamana yetu

Angelica Pesha ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mixx by Yas Tanzania.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *