Nchini Niger, asilimia 57 ya wananchi wana uwezo wa kufikia kituo cha afya kilichoko kwenye eneo la kilometa 5 kutoka makazi yao.

Wananchi waliobakia wanaishi maeneo ya ndani zaidi na hivyo huduma bora za afya zinasalia kuwa mtihani mkubwa.

Mathalani hapa mji wa Dosso, kilometa 130 kusini-mashariki mwa Niamey, mji mkuu wa Niger, huduma ziko  mbali.

Video ya WHO inaonesha gari linafika tayari kutoa huduma za afya. Gari hili ndio linaitwa kliniki tembezi kwani linafikisha huduma za afya pale waliko wananchi.

Nana Sakina Ibrahim ni mratibu wa huduma hii katika shirika la kiraia la Tattalin Rayuwa.

“Huduma za kliniki tembezi zinasaidia kuleta wananchi wanaoishi mbali na vituo vya afya kupata huduma na hivyo kuongeza idadi ya utoaji huduma za afya. Kliniki zinatoa huduma za uzazi kama vile kwa mama na mtoto, vile vile utapiamlo, chanjo na ushauri wa tiba. Hii inasaidia kubaini changamoto mapema na hivyo kutoa tiba sahihi.”

Kikundi cha wanawake na watoto wamekusanyika karibu na mhudumu wa afya wa WHO katika kliniki tembezi nchini Niger.

Kikundi cha wanawake na watoto wamekusanyika karibu na mhudumu wa afya wa WHO katika kliniki tembezi nchini Niger.

Kupitia wahisani, WHO imepatia mafunzo wataalamu wa afya na watendaji wa kijamii ambapo katika mji wa Dosso na Fillingue, kusini-magharibi mwa Niger wataalamu wa afya 16 na wahudumu wa kijamii 40 wamepatiwa mafunzo.

Video ya WHO inawaonesha wataalamu wa afya wakiwasili kijijini na mhudumu wa kijamii Haoua Amadou akiwa na kipaza sauti anatangaza..

Anasema njooni jamani kwenye kituo cha kupata huduma Nguide. Timu tembezi iko hapa kwa ajili ya huduma za afya, mashauriano na hata chanjo. Mtoto asiye na chanjo yuko hatarini kupata  magonjwa.

Wito umeitikiwa na Sakina Boureima mama mjamzito na anasema,

“Nimekuja hapa kwa huduma ya uchunguzi kabla ya kujifungua. Nina furaha kwa sababu niña afya, vivyo hivyo kwa ujauzito wangu. Ni nafuu kubwa kwa sababu timu  hii imekuja kijijini kwetu.”

Dkt. Mamane Sami Mahamane ni Mkurugenzi wa Kanda wa Afya na Usafi wa Umma eneo la Dosso nchini Niger na anasema,

« WHO ni moja ya washirika ambao kila mara wako nasi kusaidia kuhamasisha jamii na kutoa huduma bora za afya. « 

Kwa msaada huu, WHO inatekeleza wito wa kutomwacha yeyote nyuma katika kutekeleza lengo namba 3 la Malengo ya Maendeleo Endelevu, SDG kuhusu afya bora kwa wote.

Mwaka 2024 na 2025 watu milioni 2 nchini Niger walinufaika na huduma za kliniki hizo tembezi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *