Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stéphane Dujarric akizungumza na waandishi wa habari jijini New York, Marekani amesema tukio hilo limefanyika kati ya tarehe 12 na 19 mwezi huu wa Januari chanzo kikiwa ni mapigano na mashambulizi dhidi ya raia.

Akinukuu mashirika ya Umoja wa Mataifa ya kiutu nchini DRC, Dujarric amesema hali hiyo ya ukosefu wa amani sio tu jimboni Kivu Kaskazini bali pia jimboni Kivu Kusini na kwamba “watu wanalazimika kukimbia makwao na shughuli za kibinadamu zinakwama.”

Uvira nako raia wauawa

Huko mjini Uvira jimboni Kivu Kusini, mashirika ya kiraia ya eneo hilo yanaripoti kuwa takribani raia 12 wameuawa na makundi yaliyojihami tangu tarehe 18 mwezi huu wa Januari.

“Na kutokana na hofu ya kuendelea kwa vurugu hizo, takriban watu 2,400 wamekimbia mji wa Uvira kuelekea Kamanyola, ambako wamehifadhiwa na wenyeji wao, na wengine wakiwa kwenye vituo vya pamoja wakitafuta usalama,” amesema Dujarric akiongeza kuwa mahitaji yao ya dharura zaidi ni pamoja na chakula, makazi, maji, huduma za usafi wa mazingira na usafi binafsi, ulinzi, na huduma za afya.

Amesisitiza kuwa upatikanaji wa misaada ya kibinadamu, “kama mnavyoweza kufikiria, unaendelea kuwa changamoto jimboni Kivu Kusini, hasa katika eneo la Fizi, ambako barabara nyingi muhimu zimefungwa kutokana na ukosefu wa usalama. Hali hiyo imetatiza shughuli za kibinadamu, ikiwemo usambazaji wa vifaa vya matibabu kwa ajili ya kukabiliana na mlipuko wa kipindupindu.”

Jaribio la kupora bidhaa za kiutu Baraka

Siku ya Jumatano ya wiki hii, huko Baraka, “watu wenye silaha waliingia katika baadhi ya majengo ya washirika wetu wa kibinadamu. Waliwatishia wafanyakazi na kujaribu kupora  vifaa vya usaidizi wa kiutu.”

Dujarric amesema wanalaani vikali mashambulizi yote dhidi ya raia na vitisho dhidi ya wafanyakazi wa kibinadamu. 

“Tunazitaka pande zote kuheshimu wajibu wao chini ya sheria ya kimataifa ya kibinadamu, ikiwa ni pamoja na kuwalinda raia, kulinda miundombinu ya kiraia, na kuwezesha utoaji wa msaada wa kibinadamu kwa usalama, bila vikwazo na kwa haraka.”

Mapema wiki hii iliripotiwa kuwa waasi wa M23 wameondoka mji wa Uvira na kwamba serikali ya DRC imeanza mkakati wa kuimarisha mamlaka za dola kwenye mji huo ulio jimboni Kivu Kusini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *