
Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu (OCHA) imetangaza katika ripoti yake kwamba mwaka jana (2025) walowezi na jeshi la Israel waliua Wapalestina 240 katika Ukingo wa Magharibi.
OCHA imeongeza kuwa: Mwaka 2025, raia elfu nne wa Palestina pia walijeruhiwa kwa kupigwa risasi wanajeshi wa jeshi la Israel katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mnamo 2025, zaidi ya Wapalestina 37,000 wa Ukingo wa Magharibi walilazimika kuhama makazi yao kutokana na kuharibiwa nyumba zao.
Ripoti hiyo inaongeza kuwa katika kipindi hicho hicho, walowezi wa Kizayuni waliwashambulia Wapalestina wanaoishi katika Ukingo wa Magharibi na mali na milki zao mara 1,828.
Umoja wa Mataifa umeendelea kuwa: “Utawala wa Israel umebomoa nyumba 256 na miundombinu ya Wapalestina katika kipindi hicho hicho.”
Ripoti hiyo imesema, takriban familia 100 za Wapalestina zimelazimika kuhama makazi yao katika wiki mbili tu za mashambulizi ya walowezi wa Kizayuni.
OCHA imesema, “Mwaka jana, ubomoaji wa majengo ya Wapalestina katika mji unaokaliwa kwa mabavu wa Quds kwa kisingizio cha kutokuwa na kibali cha ujenzi uliongezeka kwa kiwango kisicho cha kawaida.”
Itakumbukwa kuwa, wanajeshi wa Israel huvamia nyumba na mashamba ya Wapalestina wanaoishi katika Ukingo wa Magharibi kila siku, na eneo hilo linashuhudia wimbi la mivutano na mapigano ya uwanjani kati ya Wapalestina na wanajeshi wa Israel, pamoja na uvamizi katika vitongoji na kukamatwa ovyo kwa Wapalestina.