Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer ametaka Rais wa Marekani Donald Trump aombe radhi kwa madai yake kwamba wanajeshi wa Ulaya hawakuwa mstari wa mbele katika vita vya kivamizi vya mwaka 2001 vilivyoanzishwa na Marekani na waitifaki wake dhidi ya Afghanistan.

Katika kauli ya ukemeaji wa moja kwa moja kufanywa kwa nadra dhidi ya rais wa Marekani, Starmer amesema, maoni aliyotoa kabla Trump kwa mtangazaji wa chaneli ya televisheni Marekani ya Fox News kwamba washirika wa NATO walibaki “nje kidogo ya mstari wa mbele” nchini Afghanistan yalikuwa “ya matusi na ya kutisha hasa”.

Alipoulizwa kama angetaka Trump aombe radhi, Starmer alisema, “kama mimi ningesema vibaya kwa njia hiyo au kusema maneno hayo, bila shaka ningeomba msamaha.”

Waziri Mkuu wa Uingereza amewaenzi pia wanajeshi 457 wa nchi hiyo waliouawa baada ya kujiunga na uvamizi wa kijeshi dhidi ya Afghanistan ulioongozwa na Marekani mwaka 2001 kwa kisingizio cha mashambulizi ya Septemba 11 dhidi ya nchi hiyo.

Wakati huohuo, Ikulu ya White House imetoa taarifa ya kupinga ukosoaji wa kiongozi wa Uingereza dhidi ya Trump.

“Rais Trump yuko sahihi kabisa – Marekani imefanya mengi zaidi kwa NATO kuliko yaliyofanywa na nchi nyingine yoyote katika muungano huo yakichanganywa pamoja,” ameeleza msemaji wa Ikulu ya White House Taylor Rogers katika taarifa iliyotumwa kwa shirika la habari la AFP.

Zaidi ya wanajeshi 150,000 wa Uingereza walihudumu nchini Afghanistan, na kuifanya nchi hiyo kuwa mchangiaji wa pili kwa ukubwa katika muungano vamizi wa kijeshi ulioongozwa na Marekani dhidi ya nchi hiyo kwa kisingizio cha kuuangamiza mtandao wa al-Qaeda na vikosi vya wanamgambo wa Taliban…/

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *