Harakati ya muqawama ya Palestina, Hamas, imelaani jinai mpya ya utawala mhalifu wa Israel, ikisema kuwa wanajeshi wa Israel wamefukua mamia ya makaburi katika eneo la mashariki la Ukanda wa Gaza unaozingirwa. Wanajeshi wa utawala wa Kizyauni wamefukua makaburi ya Wapalestina wakitafuta mwili wa mateka wa mwisho wa utawala huo.

Msemaji wa Hamas, Hazem Qassem amesema kuwa: “Uvunjaji sheria huo na kukiukwa maadili kulikofanywa na Wazayuni vinashuhudiwa kwa sababu tu mfumo wa kimataifa unakataa kuuwajibisha utawala huo kwa jinai kubwa ulizofanya ambazo hazijawahi kushuhudiwa katika zama hizi.”

Msemaji wa Hamas amesema haya baada ya taarifa ya Euro-Med Human Rights Monitor ambayo imetaja ufukuaji mkubwa wa makaburi unaofanywa na jeshi la Israel mashariki mwa mji wa Gaza kwa kisingizio cha kutafuta mwili wa mateka wake wa mwisho, kuwa ni ukiukaji mkubwa wa misingi ya ubinadamu. 

Taasisi hiyo ya Ulaya imesisitiza kuwa hatua ya Israel ya kuhalalisha kufukua makaburi ya Wapalestina huko Gaza haiwezi kutetea kukiukwa utukufu wa maeneo ya mazishi ya Wapalestina au kufukua mabaki ya miili ya wafu. 

Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, Israel imeharibu kwa mpangilio maalumu makaburi ya Waislamu katika Ukanda wa Gaza na kuivunjia heshima miili pamoja na kuhamisha makumi ya mabaki.

Juzi Jumatatu jeshi la Israel lilidai kuwa limepata mabaki ya mwili wa Ran Gvili, mateka wa mwisho wa utawala huo aliyekuwa akishikiliwa katika Ukanda wa Gaza na kuyasafirisha hadi katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu. 

Katika hujuma hiyo mabaki ya miili ya Wapalestina yaliachwa juu bila ya kupewa heshima inayostahiki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *