Katika miaka ambayo Uingereza ilijiona kuwa taifa kubwa na lisilo na mpinzani duniani, ardhi moja katika Afrika Mashariki polepole ikageuka na kuwa eneo la mojawapo ya uzoefu mchungu zaidi wa kikoloni.

Kenya, ambayo ilianza kama kituo cha biashara tu kwenye njia ya reli ya Uganda, mara moja ikabadilika na kuwa maabara ya sera za utumiaji mabavu na ubaguzi za Waingereza, ambazo zilianza kwa unyakuzi wa ardhi yenye rutuba, utwishaji wa sheria za ubaguzi wa rangi, na kuwabadilisha wenyeji kuwa watumwa, na hatimaye kupelekea kuibuka mlipuko wa kijamii ambao umebakia katika historia kama Harakati ya Mau Mau. Harakati hii haikuzaliwa kutokana na vurugu za upofu, bali kutokana na miongo kadhaa ya dhulma, udhalilishaji, na kunyang’anywa mali; na mjibizo wa Waingereza kwake ulikuwa mojawapo ya ukandamizaji wa umwagaji damu zaidi wa kikoloni wa karne ya 20.

Kuanzia mwishoni mwa karne ya 19, Uingereza ilipoingia Afrika Mashariki kama sehemu ya ushindani wa ukoloni wa Ulaya, Kenya polepole ikawa moja ya makoloni muhimu zaidi ya ukoloni. Uwepo wa Uingereza ulianza kwa kudhibiti njia za biashara na kuanzisha vituo vya utawala, lakini kwa kuujengwa reli ya Uganda, ambayo ilianzia Mombasa hadi Ziwa Victoria, satwa ya kijeshi na utawala wa Uingereza ukaimarisha na kukita mizizi. Baada ya reli kukamilika, kwa haraka Uingereza ikaanza kufuatilia lengo lake kuu: Kunyakua ardhi yenye rutuba ya Kenya na kuzigeuza kuwa mashamba makubwa kwa walowezi wa Ulaya. Sera hii, ambayo baadaye ilijulikana kama “nyanda za juu za wazungu,” ilichukua mamilioni ya hekta za ardhi bora ya kilimo kutoka kwa watu wa asili, haswa Wakikuyu, na watu wa asili, ambao walikuwa wameishi katika ardhi hizi kwa vizazi vingi, ghafla wakawa “walowezi na wakazi haramu” katika ardhi yao wenyewe. Wenyeji walilazimishwa kuwa wafanyakazi wa bei rahisi katika mashamba ya Wazungu au kuishi katika maeneo ya mbali, yasiyoendelea yaliyotengwa kwa ajili yao na wakoloni.

Sambamba na unyang’anyi huu mkubwa, Uingereza ilianzisha mfumo wa sheria za kibaguzi zilizolenga kudhibiti kikamilifu nguvukazi ya Waafrika. Kodi kubwa, sheria za kufanya kazi kwa lazima, mibinyo ya kutembea na sharti la kubeba kitambulisho kilichojulikana kama “kipande” zilikuwa zana zilizowaweka watu katika umaskini na utegemezi. Waafrika walitengwa katika ushiriki wa kisiasa na walikuwa na ufikiaji mdogo wa elimu na kazi nzuri. Mchanganyiko huu wa mashinikizo, pamoja na udunishaji wa kiutamaduni na ubaguzi, polepole uliisukuma jamii ya Wakenya kuelekea malalamiko makubwa na hasira iliyofichwa. Kwa vijana wengi wa Kikuyu, ambao hawakuwa na ardhi wala mustakabali mzuri, upinzani ulikuwa njia pekee ya kurejesha heshima na haki yao ya kuishi.

Moja ya vituo vya kuwashiklia Wakenya katika kipindi cha ukoloni wa Uingereza

Katika mazingira haya, harakati ya Mau Mau iliibuka, harakati iliyojikita katika mitandao ya kitamaduni, viapo vya pamoja, na hamu ya kurejesha ardhi. Kwa hakika, Mau Mau ilikuwa harakati ya kisiasa na kijamii ambayo ililenga kukomesha utawala wa kikoloni na kurejesha ardhi zilizoporwa na mkoloni. Baada ya harakati za Mau Mau kushika kasi, Uingereza ilitangaza hali ya hatari mnamo 1952 na kuanza ukandamizaji ambao baadaye uliondokea kuwa mojawapo ya vipindi vya kikatili na giza zaidi katika historia ya ukoloni.

Wakati wa hali ya hatari, maelfu ya watu walikamatwa bila kufunguliwa mashtaka, wengi wao hawakuwa na uhusiano wowote na Mau Mau na walikamatwa kwa sababu tu ya kuwa kwao Wakikuyu au kuishi katika maeneo yenye kutiliwa shaka. Kukamatwa huku kulikuwa mwanzo wa mtandao wa kambi za kazi ngumu ambapo wafungwa walishikiliwa katika hali zisizo za kibinadamu. Nyaraka zilizotolewa na serikali ya Uingereza mwaka wa 2011 zinaonyesha kwamba mateso katika kambi hizi hayakuwa ya kipekee bali yalikuwa ya kimfumo. Wafungwa walipigwana kuteswa vibaya, kufa njaa, kunyimwa usingizi, kufanyishaa kazi ngumu, na hata kushambuliwa kingono. Katika Kambi ya Hola, mojawapo ya vituo maarufu vya kushikilia watu, kwa akali wafungwa 11 walipigwa hadi kufa na walinzi katika siku moja, tukio ambalo baadaye likawa nembo ya utimiaji mabavu ya mkoloni Muingereza.

Wanaharakati wa Mau Mau walipokuwa wakipigania haki zao

Mauaji ya halaiki pia yalikuwa sehemu ya sera ya ukandamizaji. Zaidi ya wanachama 1000 wa Mau Mau waliuawa baada ya kesi fupi na mara nyingi zisizo za haki, moja ya idadi kubwa zaidi ya mauaji ya kisiasa katika historia ya ukoloni. Zaidi ya hayo, maelfu waliuawa katika operesheni za kijeshi, mashambulizi ya anga, usafishaji wa vijiji na mapigano ya hapa na pale. Makadirio yanaweka jumla ya waathiriwa, wakiwemo wapiganaji na raia, kuwa zaidi ya 15,000. Vurugu hizo hazikuishia kwenye uwanja wa vita pekee; bali familia ziligawanyika vipande vipande, vijiji viliharibiwa, na miundo ya kijamii ya kitamaduni ya watu wa Kikuyu iliharibiwa vibaya.

Licha ya ukandamizaji mkali, Harakati ya Mau Mau ilikuwa na athari kubwa katika mchakato wa uhuru wa Kenya. Ingawa harakati hiyo ilishindwa kikamilifu mwaka wa 1960, lakini upinzani wao ulifungua njia ya uhuru wa Kenya mwaka wa 1963. Miongo kadhaa baadaye, manusura wa kipindi hicho waliwasilisha kesi dhidi ya serikali ya Uingereza, wakidai fidia sambamba na kuitaka serikali ya London ikiri rasmi kuhusika katika sakata hilo. Mnamo 2013, baada ya kutolewa kwa hati za siri na shinikizo la kisheria, serikali ya Uingereza ililazimika kukiri rasmi. Kukiri huku kwa kuchelewa kunaonyesha kwamba, ukatili uliofanywa wakati wa ukandamizaji wa Mau Mau haukuwa matukio ya hapa na pale bali sehemu ya sera iliyopangwa ya vurugu na ukandamizaji.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *