Nimekuwa nikifuatilia katika mitandao ya kijamii hasa kunapokuwa na taarifa za kifo kiongozi wa Serikali, Polisi au hata mbunge anayetokana na CCM, wapo watu wanalipuka kwa furaha, huu sio utu wala utamaduni watanzania wa Nyerere.

Kuna kitu ambacho hakiko sawa na ni Serikali ya chama tawala, Chama cha Mapinduzi (CCM) na chama chenyewe ndio wamebeba dhamana ya kurejesha upendo, umoja na mshikamano wa Watanzania ambao unatoweka kwa kasi.

Mifano ni mingi kwani hata Agosti 6, 2025 kulipotangazwa taarifa za kifo cha aliyekuwa Spika wa Bunge la 12, Job Ndugai wapo watu walifurahia na Desemba 2024 kulipotoa ajali iliyohusisha basi lililobeba wabunge, wapo watu walifurahia.

Walipofariki wabunge wawili, mbunge wa Viti maalum, Halima Idd Nassoro, Januari 18, 2026 Jijini Dar es Salaam na Mbunge wa Peramiho, Jenister Mhagama Jijini Dodoma Desemba 11,2025, hali ilikuwa hivyo hivyo kwenye mitandao.

Polisi wetu 8 walipouawa kule Kibiti mwaka 2017 hali ilikuwa hivyo hivyo, leo polisi au kiongozi wa Serikali akipata ajali au madhila yoyote wapo Watanzania wenzetu wanafurahia, hawa sio Watanzania tuliokuwa nao kabla ya mwaka 2016.

Sisi Watanzania kabla ya 2016, tulikuwa mtu yeyote akifariki awe ni kiongozi, Mtanzania wa kawaida tulikuwa tunaomboleza pamoja lakini leo kuna makundi kwamba wakifa hawa tunasikitika, lakini wakifa wale tunashangilia. Si sawa.

Tutakiwa watu tusiojitambua kama tutapuuzia yale yanayoendelea katika mitandao ya Kijamii X (Twitter), Tiktok, Facebook, Instagram na Whatsapp wakati tukitambua fika tuko kwenye kizazi cha kidigitali na sehemu kubwa ni vijana.

Ukisoma Ripoti ya Takwimu ya Sekta ya Mawasiliano Robo ya mwaka inayoishia Desemba 2025 iliyotolewa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inaonyesha watumiaji wa Intaneti hapa Tanzania imefikia milioni 58.1.

Sumu ya chuki na visasi tunayoishuhudia katika mijadala ya vijana huko Tiktok, Club House na X Space haina afya kwa taifa letu na ndio maana nasema Serikali ya CCM ina dhamana kubwa kulirudisha taifa pamoja kama kabla ya 2016.

Kitendo cha baadhi ya watanzania kufurahia madhila yanayoyapata makundi niliyoyaeleza ni dhahiri tatizo lipo katika uendeshaji wa nchi ambayo kwa sasa iko chini ya CCM, na ndio yenye dhamana ya kuturejeshea upendo uliotoweka.

Lakini kabla ya kuurejesha ni lazima tukiri kuna mahali tumeteleza, bila kufanya hivyo na tukaendelea kushupaza shingo, kuhamishia lawama kwa mabeberu au kutoa kauli za kejeli badala ya kuponya, upendo tunaoulilia hautarudi.

Tuliteleza wapi? Kwa mtizamo wangu tatizo lilianza pale tulipoanza kuwabagua watanzania kwa itikadi zao za kisiasa, yaani tukafika mahali tukatamka wazi wazi kuwa mkichagua diwani au mbunge wa upinzani basi maendeleo hakuna.

Tuliyafanya haya wakati tukitambua kabisa kuwa Ibara ya 13(1) ya Katiba inasema Watu wote ni sawa mbele ya sheria, na wanayo haki, bila ya ubaguzi wowote, kulindwa na kupata haki sawa mbele ya sheria. Tulivunja Katiba wazi wazi.

Tulienda mbali na kuzuia mathalan wabunge wa CCM kumtembelea gerezani mbunge wa Arusha mjini wakati ule Godbless Lema na Tundu Lissu alipokuwa hospitali kule Nairobi. Wapo wachache sana waliokuwa na uthubutu.

Ndio kipindi tukaanza kushuhudia kesi za kisiasa zikifunguliwa dhidi ya viongozi wa upinzani bila kufikiria kuwa mathalan, vyama hivyo vina wanachama na wafuasi wengi na nyuma yao kuna kundi kubwa la watu wanaowaunga mkono.

Tukazidi kupalilia chuki kwa kukandamiza haki katika chaguzi zetu zote zilizofanyika mwaka 2019,2020,2024 na 2025 na baya zaidi tukatumia utekaji na kupoteza watu na mauaji ya wenye maoni tofauti na watawala, kama ndio silaha ya kisiasa.

Tunashuhudia ukamataji holela (arbitrary arrest) unaofanywa na Polisi na vyombo vingine vyenye mamlaka ya ukamataji, watu wanawekwa mahabusu zisizojulikana na hata ndugu wanapoulizia wanaambiwa hawapo wakati sheria zipo.

Sasa maandamano yale ya Oktoba 29,2025 yaliyoambana na vurugu hayakuja tu hivi hivi na wala siamini kama vyombo vyetu vya usalama vilikuwa havioni likija, kwa sababu lilikuja kutokana na mkusanyiko wa hasira ya muda mrefu. Ili turudi kuwa wamoja, tunaopendana, kujali utu wa kila mtu na wenye mshikamano ni lazima viongozi wetu wa Serikali ya CCM wajishushe na kukiri kutoka moyoni kuna mahali tumekosea, tujisahihishe na tufungue ukurasa mpya.

Daniel Mjema ni mwandishi wa habari na mwanafunzi wa Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Mawasiliano ya Umma, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania. 065660090

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *