
Kila ninapofuatilia mijadala na maelezo ya wananchi wanapotembelewa na viongozi au waandishi wa habari kupata maoni juu ya masuala makubwa ya kijamii yanayojitokeza, jambo linaloibuka mara kwa mara ni kutofuatwa kwa sheria au kuwepo kwa watu wanaoonekana kana kwamba sheria zilizopo haziwagusi.
Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC), ambalo linafanya kazi kama idara ya serikali na si taasisi ya umma kama sheria inavyoelekeza, utawasikia wananchi wanapopewa nafasi kuelezea kero wanazopambana nazo wakilalamikia matumizi mabaya ya sheria.
Miongoni mwa maeneo yanayolalamikiwa ni upandishaji holela wa kodi, ada, tozo na malipo yaliyopewa majina mbalimbali, hali ambayo imesababisha maisha kuwa magumu na kuwaumiza zaidi wanyonge wenye kipato duni.
Kinachowashangaza watu ni kwamba alipoingia madarakani baada ya uchaguzi uliokuwa na utata mwaka 2020, Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, alisema yeye si muumini wa viwango vikubwa vya kodi.
Hii ni kwa sababu viwango vikiwa vya wastani watu hawaoni tabu kulipa, lakini vikiwa vya juu hutafuta njia za mlango wa nyuma au hata kupitia dirishani kukwepa wanapobanwa.
Matokeo yake, rushwa hupata mwanya wa kushamiri na serikali kukosa fedha za kugharamia miradi na huduma za kijamii.
Kinachoonekana kila kukicha ni kodi na ada kuendelea kupanda juu zaidi, huku watu wakilalamika kuwa mfumuko wa bei ni mkubwa na mzigo wa kodi, ada, tozo au mchango ni mkubwa na haubebeki.
Kwa mfano, hivi karibuni serikali imekuja na namba mpya za vyombo vya moto na kuwataka wamiliki kubadilisha. Matarajio ya wengi yalikuwa kwamba gharama ingekuwa kati ya shilingi 20,000 hadi 30,000 ili kupata usajili.
Hata hivyo, kiwango kilichowekwa cha sh85,000 kwa gari na Sh55,000 kwa pikipiki, kinalalamikiwa kuwa kikubwa na haieleweki ni kigezo gani kilitumika kufikia kiwango hicho. Hapa kinacholalamikiwa ni kwamba sheria na kanuni zilizopo zinatumiwa vibaya na wanaosimamia utekelezaji wake.
Vilevile, serikali imepandisha kodi kwa zaidi ya asilimia 20 kwa maduka yaliyoko katika majengo ya serikali na yale yaliyotaifishwa baada ya Mapinduzi ya 1964. Hatua hii imegusa zaidi Soko Kuu la Darajani na maeneo ya biashara yaliyo karibu na soko hilo.
Bila shaka ongezeko la kodi, kiwango kikubwa cha ada ya usafi na ukizingatia wanaodaiwa kutokuweka mazingira safi kutozwa faini kubwa, wafanyabiashara watalazimika kufidia gharama hizo kupitia bidhaa wanazouza, iwe ni nguo, chakula, nyama, samaki au matunda.
Vilevile, yapo malalamiko juu ya utoaji wa zabuni za miradi na maeneo ya huduma kama vile maeneo ya kuegesha magari. Hili linadaiwa kukosa uwazi na madai haya hayafai kupuuzwa kwa kuwa uwazi ni kigezo kikubwa cha utawala bora.
Ni kawaida unapowadia mwezi wa Ramadhani kusikia viongozi wa serikali wakiwaomba wafanyabiashara wasiuone mwezi huu kama wa kuchuma kwa kuongeza bei za bidhaa, bali kuwa mwezi wa ibada. Katika hili, serikali ingeonyesha mfano kwa nayo kuwaonea huruma wafanyabiashara.
Eneo jingine la sheria linalolalamikiwa ni namna serikali inavyoshughulikia majengo yanayovunjwa ili kupisha upanuzi wa barabara kuu.
Baadhi ya watu wanalalamika kuwa fidia ni ndogo na malipo yake ni mtihani, wakitaka suala hilo lipatiwe ufumbuzi kabla ya bomoa-bomoa kufanyika.
Nyumba zilivunjwa au kumegewa sehemu, na pia ilihusisha vibanda vya biashara ambavyo wamiliki walivipatia leseni wiki chache kabla ya zoezi la kuvunja kufanyika.
Swali linaloulizwa ni kwa nini walitozwa ada ya leseni ikiwa vibanda vyao vilikuwa tayari katika mpango wa kuvivunja na kwa nini walikatiwa leseni za biashara au kuruhusiwa kufanya shughuli wiki chache kabla ya bomoa-bomoa?
Kupitia ZBC Radio na mikutano mbalimbali, wananchi wanalalamika kuwa majengo ya wanyonge yamevunjwa, lakini ya wakubwa hayakuguswa kwa sababu walikataa majengo yao yasivunjwe mpaka walipwe fidia wanayoiona inastahiki.
Hapa mtu anajiuliza je, sheria za Zanzibar zimetungwa kwa ajili ya wanyonge pekee, na wale wanaoitwa waheshimiwa, mabwana wakubwa au mabibi wakubwa hazihusu?
Kwa bahati mbaya, suala hili halikutolewa maelezo, na kama ingekuwepo nafasi ya waandishi wa habari kumtaka Rais Mwinyi afafanue, ingesaidia sana.
Aidha, mikutano ya kila mwezi iliyosaidia sauti za wanyonge kusikika, iliyoanzishwa na Rais Mwinyi alipoingia madarakani mwishoni mwa mwaka 2020 na kusema ni endelevu, imetoweka kama moshi hewani.
Serikali inapaswa kuitafakari hali hii na kufanya uamuzi utakaoshirikisha maoni ya wananchi, badala ya kuja na uamuzi kwa imani kuwa una nia njema, ilhali wananchi wanahisi yanawaumiza.
Serikali sikivu na inayoweka umuhimu kwa amani na utulivu hujali wananchi wanapolalamika, kwa sababu amani na utulivu hujengwa pale ambapo watu wanaona sheria hazipindwi na zinatekelezwa kwa busara, bila ubaguzi au viashiria vya maonevu.