Serikali ya Somalia imesema kuwa msaada wa chakula uliotolewa kwenye ghala wakati wa shughuli za upanuzi wa bandari katika mji mkuu, Mogadishu, umerejeshwa kwa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), kufuatia ripoti kwamba maafisa wa eneo hilo wamekamata msaada wa chakula uliotolewa na nchi wafadhili.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Somalia imesema kuwa bidhaa za chakula zilizotolewa ghalani zimerejeshwa zote kwa shirika la WFP na kwamba serikali inawajibika kikamilifu kwa hali hiyo ya kusikitisha. 

Itakumbukwa kuwa mapema mwezi huu Marekani ilisisitisha misaada yote kwa serikali ya Somalia ikidadi kuwa maafisa wa nchi hiyo wameharibu ghala la WFP lililofadhiliwa na Marekani na kwamba walikamata kinyume cha sheria tani 76 za msaada wa chakula uliotolewa na  wafadhili kwa ajili ya wananchi wa Somalia walio katika mazingira magumu.”

Maafisa husika wa Marekani wameongeza kuwa msaada wowote wa siku zijazo utategemea uwajibikaji wa Serikali ya Shirikisho la Somalia.

Juzi Jumatatu serikali ya Somalia ilisema kuwa imeipatia WFP ghala kubwa na linalofaa zaidi ndani ya eneo la Bandari ya Mogadishu ili kuboresha uwezo wa kuhifadhi na ufanisi wa usambazaji wa chakula.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Somalia awali ilisema kuwa ghala lililoko ndani ya eneo la Bandari ya Mogadishu halikuathiriwa na shughuli zinazoendelea za upanuzi wa bandari.

Somalia na Marekani zimekuwa katika mvutano katika miezi ya karibuni huku Washington ikiwashambulia raia wa Somalia wanaoishi Marekani.

Mwezi Novemba mwaka jana, Rais Donald Trump wa Marekani alisitisha hadhi ya muda ya ulinzi kwa wahamiaji wa Kisomali, akiwatuhumu kuwa vurugu za magenge. Trump alisema Wasomali wanaoishi Marekani wanapaswa kurejeshwa nchini kwao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *