Makala ya uchambuzi iliyochapishwa na gazeti la Uingereza la The Guardian imefafanua ilichokielezea kuwa ni eneo la kutisha huko Minneapolis, Minnesota, nchini Marekani na kusema kwamba ni wakati muhimu unaofichua sura ya ufashisti wa wazi chini ya utawala wa Rais Donald Trump.
Katika mitaa ya jimbo hilo, David Smith, mkuu wa ofisi ya Washington ya gazeti la The Guardian, ameshuhudia mazungumzo kati ya polisi wawili wa Shirikisho mmoja akimwambia mwingine – wote wawili wakiwa wamewaelekezea waandamanaji silaha zao – kwamba: “Hali hii inashabihiana na mchezo wa Call of Duty. Inashangaza sana, sivyo?”
Mwandishi huyo amechora picha kamili ya alichokielezea kama ufashisti katika enzi ya Trump, huku polisi hao wawili wakikabiliwa na umati wa watu wenye hasira siku ya Jumamosi kufuatia mauaji yaliyofanywa na maafisa wa Idara ya Forodha dhidi ya raia wa Marekani, Alex Pretty katika eneo ambalo si mbali na mahali alipouliwa Renee Nicole Good mnamo Januari 7, ambalo nalo halikuwa mbali na eneo ambako George Floyd aliuawa na polis wa Marekani mwaka 2020.
Mwandishi wa gazeti la The Guardian la Uingereza ameeleza kuwa, kupelekwa maafisa wa uhamiaji na forodha waliojuzatiti kwa silaha nyingi katika jiji kubwa, wakiwa wamevaa barakoa na fulana za kujikinga na risasi, kumetengeneza mandhari ya kutisha inayoshabihiana na ya vita vya wenyewe kwa wenyewe.”

Ameeleza kwamba kampeni hiyo si ya sadfa, bali Trump analenga miji inayoongozwa na Wademokrati na Wamarekani weusi, katika mfumo wa “adhabu ya pamoja” ya kisiasa, kwa namna ya tawala za kimabavu zinazotumia nguvu za kisiasa kuwakandamiza wapinzani.
Uchambuzi huo umeongeza kuwa Minnesota imekuwa uwanja wa kulipiza kisasi cha kisiasa, kwani ni jimbo ambalo Trump amepoteza mara kwa mara, lina jamii kubwa zaidi ya Wasomali nchini Marekani, na lina wanasiasa wanaomkasirisha, kama mbunge Ilhan Omar, pamoja na kumbukumbu ya mauaji ya George Floyd yaliosababisha maandamano ya Black Lives Matter (Maisha ya Watu Weusi Muhimu).