Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amekiri kuwa sheria ya msituni ndiyo inayotawala hivi sasa duniani na kusisitiza kwamba kuna udharura wa kufanyika mageuzi katika Baraza la Usalama la umoja huo.

Pars Today imeripoti kuwa, Guterres amesema, badala ya utawala wa sheria, tunashuhudia sheria ya msituni ikitawala duniani, na akatamka kwa mara nyingine tena kwamba, kulifanyia mageuzi Baraza la Usalama ni jambo lenye udharura; na nchi zote zinapaswa ziiheshimu Mahakama ya Kimataifa ya Haki na kutekeleza kikamilifu maamuzi yake yenye ulazima bila kuchagua.

Katibu Mkuu wa UN, -ambaye siku ya Jumatatu ya Januari 26 alihutubia mkutano wa Baraza la Usalama uliofanyika kwa anuani: “Sisitizo la Kutawala Sheria za Kimataifa na Njia za Kuimarisha Amani, Haki na Ushirikiano wa Pande Kadhaa-,” aliongezea kwa kusema: “kutawala sheria ndilo jiwe la msingi wa kupatikana amani na usalama wa kimataifa, ufunguo wa kuwepo uhusiano wa kirafiki baina ya nchi na maeneo yote duniani na moyo unaotuta wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa”.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, mnamo mwaka 2024, nchi wanachama zilipitisha Mkataba wa “Mustakabali”, ambao ulijumuisha ahadi ya kufanya mambo kulingana na sheria za kimataifa na kutimiza kwa nia njema ahadi zinazotolewa. Lakini maneno yaliyotamkwa wakati huo hayalingani na matendo yanayofanywa hivi sasa, ambapo duniani kote, utawala wa sheria umebadilishwa kuwa sheria ya msituni. Tunashuhudia ukiukwaji wa wazi wa sheria za kimataifa na kupuuzwa kifedhuli Mkataba wa Umoja wa Mataifa. Kuhusiana na hilo, Guterres alisema: “kuanzia Ghaza hadi Ukraine, kutoka Sahel hadi Myanmar, Venezuela na kwingineko, utawala wa sheria unachukuliwa kama suala la pembeni tu. Tunashuhudia nchi zikikhalifu utawala wa sheria pasi na kuadhibiwa: kupitia utumiaji nguvu kinyume cha sheria, kulenga miundombinu ya raia, kukiuka haki za binadamu na kuzitumia vibaya, kustawisha kinyume cha sheria uundaji wa silaha za nyuklia, kuondoa tawala madarakani kinyume cha sheria na kukana haki ya utoaji misaada muhimu ya kibinadamu.”

Hotuba ya Antonio Guterres katika Baraza la Usalama, iliyotoa indhari kwamba “utawala wa sheria duniani unabadilishwa kuwa sheria ya msituni,” inaakisi hali mbaya ya mgogoro mkubwa unaotawala katika nidhamu ya dunia. Guterres alibainisha kwamba, kwa miaka 80, mfumo wa sheria wa kimataifa na Mkataba wa Umoja wa Mataifa vimezuia kuzuka Vita vya Tatu vya Dunia, lakini mfumo huohuo, sasa unazidi kupuuzwa kila uchao. Kukiri huko kwa Katibu Mkuu wa UN si utiaji chumvi wa kisiasa, bali ni ukweli unaoonekana katika maeneo mbalimbali ya migogoro na vita; kuanzia Ghaza na Ukraine hadi Sahel ya Afrika, Myanmar na Venezuela, ambapo sheria za kisheria zinatumika “kwa uchaguaji wa kiutashi kulingana na maslahi”. Mfano dhahiri na kamili wa hotuba ya Guterres ni Marekani, ambayo katika kipindi hiki, na chini ya urais wa Donald Trump, imevuka mipaka yote ya sheria na kanuni za kimataifa, na hata Mkataba wa Umoja wa Mataifa, kwa hatua zake mbalimbali haramu na za ukanyagaji wa sheria.

Kulia: Rais Nicolas Maduro wa Venezuela aliyetekwa nyara na jeshi la US ndani ya nchi yake. Na kushoto ni Trump

Sababu ya kwanza iliyomfanya Katibu Mkuu wa UN atumie istilahi hiyo nzito ya ‘sheria ya msituni’ ni kushuhudiwa ukiukaji mkubwa ambao haujawahi kushuhudiwa wa sheria za kimataifa. Guterres alizungumzia waziwazi alichokiita “ukiukwaji mkubwa mno”; unaojumuisha mashambulizi dhidi ya raia, kupuuza msingi unaokataza matumizi ya nguvu, na kutoheshimiwa ahadi juu ya masuala ya kibinadamu. Wakati serikali na makundi ya wabebaji silaha zinapoishambulia miji kwa mabomu bila ya hofu ya kuwajibishwa na zinapowawekea watu mzingiro wa muda mrefu au kutumia mabavu kwa ajili ya kubadilisha mipaka, ujumbe wa hatua hizo ni kwamba: ni nguvu, na si sheria, ndiyo inayoamua. Na hii ndio mantiki ya sheria ya msituni: kila mwenye nguvu zaidi, ndiye mwenye haki zaidi ya kutwisha matakwa yake.

Sababu ya pili ni mgogoro mkubwa unaoshuhudiwa katika mifumo ya ubebaji dhima na uwajibikaji. Guterres na wazungumzaji wengi katika mkutano huo walitilia mkazo nukta kwamba Baraza la Usalama limepooza kiutendaji katika kukabiliana na migogoro mingi, kutokana na ushindani wa madola makubwa na utumiaji wao mbaya wa kura ya turufu. Wakati chombo kinachopaswa kudhamini utekelezaji wa Mkataba wa UN kinapogeuzwa kuwa uwanja wa vuta nikuvute za kijiopolitiki, wakiukaji wa sheria hujihisi wana kinga ya kutofanywa chochote. Kukosekana ufuatiliaji athirifu katika mahakama za kimataifa, mashinikizo ya kisiasa yanayotolewa kwa taasisi za mahakama, na undumakuwili unaofanywa katika kushughulikia kesi, yote hayo yanatilia nguvu mtazamo wa kwamba, haki ni jambo la kuchagua na la kisiasa, na si la ulimwengu mzima na lisilo na upendeleo.

Na sababu ya tatu inahusiana na kutoweka imani iliyokuwepo kwa taasisi na kanuni za mahusiano ya pande kadhaa. Guterres alikumbusha kwamba, mfumo wa kimataifa umejengwa juu ya majimui ya sheria za pamoja zinazoyabana kiusawa mataifa yote “makubwa na madogo”. Lakini katika miaka ya karibuni, hatua za kujiondoa kwa upande mmoja katika mikataba, kudharau maazimio, na kudhoofisha mashirika ya kimataifa kumetuma ujumbe kwa ulimwengu kwamba majukumu ya kisheria huwa yanaheshimiwa pale tu yanapokuwa hayakinzani na maslahi ya muda mfupi ya madola yenye nguvu.

Trump na “Sheria ya Msituni”

Kutokana na yote hayo, kukiri Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa juu ya “kutawala sheria ya msituni” ni onyo na wito pia. Anachotaka kuonyesha Guterres ni kwamba, ikiwa jamii ya kimataifa haitachukua hatua ya kujenga upya imani kwa sheria za kimataifa, mageuzi ya taasisi kama Baraza la Usalama, uimarishaji wa mifumo ya uwajibikaji, na ukomeshaji wa vipimo vya undumilakuwili, dunia itaelekea upande utakaozifanya haki na usalama endelevu vipoteze maana yake…/

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *