
Katika taarifa iliyotolewa leo Alhamisi na Msemaji wake mjini New York Msrekani , Katibu Mkuu amesema kuwa wimbi la hivi karibuni la ghasia limesababisha “vifo, majeruhi na kuripotiwa kufurushwa kwa raia 180,000,” akisisitiza kuongezeka kwa hali ya ukosefu wa usalama katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo.
Bwana. Guterres pia ameonesha hofu yake kuhusu kauli za uchochezi zinazolenga jamii fulani pamoja na tangazo la kupanuliwa kwa operesheni za kijeshi, akionya kuwa hatua hizo “zitaendelea kuwadhuru raia ambao tayari wako katika hali hatarishi.”
Katibu Mkuu ameonya kuwa kuzorota kwa usalama kunazidisha mahitaji makubwa ya kibinadamu.
Raia 250,000 wamefungasha virago kukimbia vita
Kwa mujibu wa Serikali ya Sudan Kusini, raia wapatao 250,000 tayari wamekimbia makazi yao kutokana na mzozo huo katika wiki chache za mwanzo za mwaka 2026, jambo linaloonesha ukubwa na kasi ya mgogoro huo.
Akitoa wito wa hatua za haraka, Katibu Mkuu amezitaka pande zote katika mzozo kulinda raia na kuhakikisha upatikanaji salama na usio na vikwazo wa misaada ya kibinadamu.
Pia amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha “usalama wa walinda amani wa Umoja wa Mataifa, wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu na mali zao.”
Bwana. Guterres amehimiza Serikali ya Sudan Kusini na makundi ya upinzani “kuchukua hatua za haraka na za dhati kusitisha operesheni zote za kijeshi na kupunguza mvutano kupitia mazungumzo jumuishi.”
Akisisitiza kuwa hakuna suluhu ya kijeshi kwa mgogoro huo, Katibu Mkuu amesema mustakabali wa Sudan Kusini unategemea maendeleo ya kisiasa. “Mgogoro wa Sudan Kusini unahitaji suluhu ya kisiasa na si ya kijeshi,” amesema, akizitaka pande husika kukubaliana haraka juu ya ramani ya pamoja ya utekelezaji kwa mwaka wa mwisho wa kipindi cha mpito ili kuwezesha kufanyika kwa uchaguzi huru na wa kuaminika.
Amepongeza juhudi zinazoendelea za Muungano wa Afrika na Mamlaka ya Maendeleo ya Kieneo ya Afrika Mashariki (IGAD), akizihimiza nchi jirani kuongeza juhudi zao katika kuunga mkono mazungumzo jumuishi yenye lengo la kurejesha amani na utulivu katika taifa changa zaidi duniani.