
Kupitia taarifa iliyotolewa leo New York, Marekani na Naibu Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Katibu Mkuu ameonesha wasiwasi mkubwa kuhusu madhara yanayoweza kuwakumba raia, pamoja na hatari ya kurejea kwa mzozo mpana katika eneo hilo ambalo bado linaendelea kujijenga na kupona baada ya machafuko ya awali.
Tigray mzozo ulianza 2020
Mzozo huko Tigray ni kati ya jeshi la serikali ya Ethiopia na kikosi cha wapiganaji cha Tigray, TPLF, na ulianza mwezi Novemba mwaka 2020 baada ya jeshi la serikali kudai kuwa wapiganaji hao wa Tigray walishambulia kituo cha jeshi la serikali. Miongoni mwa matakwa ya Tigray ni kujitenga na Ethiopia.
Hata hivyo mwezi Novemba mwaka 2022 Sitisho la kudumu la mapigano kati ya pande mbili hizo lilitiwa Saini huko Pretoria nchini Afrika Kusini kati ya serikali ya Ethiopia na TPLF.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari, hali ya sasa inafuatia ripoti kwamba ndege zisizo na rubani zimeshambulia eneo la Tigray na kusababisha madhara huko Tigray.
Wito wa Katibu Mkuu
Katika taarifa hiyo, Naibu Msemaji huyo wa Umoja wa Mataifa Farhan Haq amesema Katibu Mkuu ametoa wito kwa pande zote zinazohusika kujizuia na kutatua tofauti zao kwa njia ya mazungumzo ya amani, pamoja na kuchukua hatua zitakazosaidia kujenga upya imani.
Amesisitiza umuhimu wa kutekelezwa kikamilifu kwa Makubaliano ya Kudumu ya Kusitisha Mapigano, akibainisha umuhimu wa kulinda mafanikio yaliyopatikana tangu mwaka 2022.
Aidha, Katibu Mkuu amethibitisha utayari wa Umoja wa Mataifa kushirikiana na Muungano wa Afrika pamoja na washirika wa kikanda ili kusaidia kuimarisha amani na utulivu wa kudumu katika eneo la Tigray.