BAADA ya aliyekuwa mshambuliaji wa Fountain Gate, Joshua Ibrahim kukamilisha uhamisho wake wa kurejea Tusker FC ya Kenya, nyota huyo amesema ni wakati wa kuangalia fursa nyingine nje ya mipaka ya Tanzania, kama ilivyokuwa pia mwanzoni.

Akizungumza na Mwanaspoti, Joshua amesema licha ya ofa nyingi alizokuwa nazo amefikia uamuzi wa kurejea katika Ligi ya Kenya aliyokuwa anaichezea hapo mwanzoni, baada ya kutumia vizuri fursa kwenye Ligi Kuu kupitia timu mbalimbali.

“Nimefanya uamuzi wa kurejea sehemu niliyokuwa mwanzo, nashukuru uongozi kwa nafasi nyingine waliyoniamini na kunipatia, mimi ni mchezaji hivyo, ninapopata fursa ninayokubaliana nayo na kuiridhia huwa ninafanya kazi popote,” amesema Joshua.

Joshua amesema kurudi kwake tena kwenye kikosi hicho cha Tusker ni ishara tosha ya uongozi kuendelea kuthamini mchango wake aliouacha kabla ya kuondoka hivyo, ni deni kubwa kwake la kuendelea kuipambania timu hiyo kwenye Ligi Kuu ya Kenya.

Nyota huyo alijiunga na Fountain Gate baada ya kuondoka Namungo aliyojiunga nayo dirisha dogo la Januari 2025, akitokea KenGold ya jijini Mbeya ambayo imeshuka daraja kwa msimu wa 2024-2025, ikitokea Ligi Kuu Bara hadi Ligi ya Championship.

Joshua alijiunga na KenGold Agosti 2024, akitokea Tusker FC ya Kenya ambapo hadi anaondoka dirisha dogo, aliifungia timu hiyo mabao manne ya Ligi Kuu, huku kwa upande wa Namungo aliyoichezea kwa miezi sita akikifungia kikosi hicho bao moja.

Katika Ligi Kuu ya Kenya, Tusker iko nafasi ya nane na pointi 27, baada ya kushinda mechi nane, sare tatu na kupoteza saba kati ya 18, ambapo safu ya ushambuliaji ya kikosi hicho imefunga mabao 16 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 18.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *