ALIYEKUWA mshambuliaji wa Singida Black Stars, Namungo FC, Mtibwa Sugar na maafande wa Tanzania Prisons, Kelvin Sabato ‘Kiduku’, yupo katika hatua za mwisho za kujiunga na KVZ ya visiwani Zanzibar, inayofundishwa na kocha, Malale Hamsini.

Nyota huyo ambaye kwa sasa yupo huru baada ya kuachana na Singida Black Stars, amefanya mazungumzo ya moja kwa moja na kocha Malale kwa ajili ya kujiunga na kikosi hicho kinachoshiriki Ligi Kuu ya visiwani Zanzibar kwa msimu huu.

Akizungumza na Mwanaspoti, Malale aliyejiunga na kikosi hicho baada ya kuondoka Mbeya City, Novemba 30, 2025, amesema ni kweli wapo katika mazungumzo hayo, ingawa kwa sasa anachosubiri ni kukamilisha baadhi ya taratibu kati ya pande mbili.

Hata hivyo, Mwanaspoti linatambua Kiduku yupo hatua za mwisho za kujiunga na KVZ, akienda kuungana na winga wa zamani wa Mbeya City, Namungo FC na JKT Tanzania, Sixtus Sabilo, aliyeachana na TMA ya Arusha inayoshiriki Ligi ya Championship.

Wachezaji hao ni pendekezo la kocha Malale ambaye amewapendekeza kwa uongozi wa kikosi hicho wasajiliwe kwa ajili ya kuongeza ushindani katika Ligi Kuu ya Zanzibar, baada ya kutokuwa na wakati mzuri tangu msimu umeanza akiwa Mbeya City.

Malale alijiunga na Mbeya City Machi 31, 2025, akichukua nafasi ya Salum Mayanga aliyejiunga na Mashujaa, ambapo kocha huyo wa zamani wa maafande wa JKT Tanzania, kwa msimu wa 2025-26, alikiongoza kikosi hicho katika jumla ya mechi tisa.

Katika mechi hizo tisa ambazo Malale aliiongoza Mbeya City, ilishinda mbili, sare mbili na kuchapwa 5. ambapo kwa ujumla kikosi hicho kilifunga mabao saba na kuruhusu 10, huku Malale akiiacha ikiwa katika nafasi ya 10 na pointi nane.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *