Dar es Salaam. Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar amepongeza ufanisi wa uendeshaji na mchango mkubwa wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), katika kuchochea maendeleo jumuishi na endelevu yanayolenga mageuzi ya sekta za kilimo, mifugo, uvuvi pamoja na viwanda vya kuchakata mazao ya kilimo nchini.
Akizungumza Leo Jumapili, Februari Mosi, 2026 wakati wa kikao na uongozi wa TADB kilichofanyika katika Ofisi za Wizara ya Fedha, Treasury Square jijini Dodoma, Waziri huyo amesema kuwa Benki imejidhihirisha kama chombo muhimu cha maendeleo ya sekta ya kilimo kutokana na mwenendo wake mzuri wa kifedha na athari chanya inayozalisha kwa wananchi.
“TADB imeonesha ufanisi wa hali ya juu katika uendeshaji wake. Taarifa ya Benki inaonesha ukuaji thabiti wa kifedha na mchango wa moja kwa moja katika kuendeleza sekta za kilimo, mifugo na uvuvi kwa manufaa ya Watanzania,”* amesema Balozi Omar.
Amesema mafanikio ya Benki hiyo yameiwezesha kuchochea uwekezaji katika viwanda vya kuchakata mazao ya kilimo, hatua inayoongeza thamani ya mazao na kupanua wigo wa ajira nchini.
Waziri wa Fedha ameshauri taasisi hiyo kuelekeza mikakati yake katika kuendeleza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara yenye ushindani mkubwa katika masoko ya kimataifa, akisisitiza umuhimu wa kuwanufaisha wakulima na wadau wa mnyororo mzima wa thamani.
“Ipo haja ya Benki kuelekeza nguvu katika mazao yenye thamani kubwa kimataifa ili kuongeza kipato cha wakulima, wafugaji na wavuvi pamoja na kukuza mchango wa sekta hizi katika uchumi wa taifa,”amesema.
Balozi Omar ameahidi Serikali kuendelea kushirikiana kwa karibu na taasisi hiyo katika utekelezaji wa mikakati yake ya muda wa kati, kwa lengo la kuongeza tija na mchango wa sekta za kilimo, mifugo na uvuvi katika kukuza uchumi wa nchi.
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa kifedha na mkakati wa muda wa kati wa Benki kwa kipindi cha mwaka 2025–2030, Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Frank Nyabundege, amesema Benki imeendelea kuimarika kifedha kwa kasi kubwa.
“TADB imekua kutoka kuwa na mizania ya shilingi bilioni 362.8 mwaka 2021 hadi kufikia shilingi trilioni 1.3 mwaka 2025, hatua inayoakisi uimara wa kifedha na ufanisi wa usimamizi wa Benki,”amesema Nyabundege.
Amepongeza tangu kuanzishwa kwake mwaka 2015, Benki hiyo imetoa mikopo yenye thamani ya zaidi ya shilingi trilioni 1.3 kwa wakulima, wafugaji na wavuvi, jambo lililochangia ongezeko la uzalishaji, ajira na maendeleo ya uchumi vijijini.
Nyabundege ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Fedha kwa kuendelea kuiwezesha Benki hiyo kwa mtaji, akieleza kuwa hatua hiyo ni uthibitisho wa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kuikuza sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi.
“Msaada wa Serikali umeiwezesha TADB kutekeleza majukumu yake kikamilifu na kuendelea kuwa chombo madhubuti cha maendeleo ya kilimo nchini,”amesema
Vilevile, ameiomba Serikali kuendelea kuipatia Benki mtaji pamoja na udhamini ili iweze kufikia masoko ya fedha ya kimataifa na kuongeza uwezo wake wa kuwakopesha wakulima na wawekezaji wa kilimo.
Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Fedha,Mshamu Ally Munde, pamoja na viongozi wengine waandamizi kutoka Wizara ya Fedha na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB).