Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei ameonya kwamba, vita vyovyote vitakavyoanzishwa na Marekani dhidi ya Iran vitageuka na kuwa vita vya kikanda.
Akihutubia mkutano na mkusanyiko mkubwa wa watu katika Husseiniya ya Imam Khomeini mjini Tehran, mkesha wa kuamkia miaka maadhimisho ya kumbukumbu ya 47 ya Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, na kumbukizi ya kurejea nchini Iran Mwasisi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Imam Khomeini, Ayatullah Khamenei amezungumzia vitisho vya hivi karibuni vya Marekani na kusema: Matamshi ya hivi karibuni ya Marekani kuhusu vita na zana za kijeshi hayana mapya.
Imam Khamenei amesisitiza kwamba, vitisho na maonyesho ya nguvu za kijeshi kamwe hayatalitisha taifa la Iran. Ameeleza bayana kuwa, “Wakati mwingine wanazungumzia vita na ndege na meli za kivita; hili si jambo jipya,” akikumbuka kwamba maafisa wa Marekani walikuwa wameitishia Iran mara kwa mara hapo awali kwa kudai kwamba “machaguo yote yako mezani, ikiwa ni pamoja na chaguo la vita.”
Katika kuakisi hotuba ya Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, vyombo vya habari vya Kiarabu vimejikita zaidi katika jibu kali la Iran kwa chokochoko yoyote, ya kukaririwa na kutokuwa na jipya vitisho vya Marekani na onyo kwamba vita yoyote dhidi ya Iran itageuka na kuwa vita vya kikanda, na kufanana matukio ya hivi karibuni na jaribio la mapinduzi.
Tovuti ya chaneli ya televisheni ya Al-Manar ya Lebanon, chini ya kichwa cha habari “Imam Khamenei: Iran haitaanzisha vita, bali itatoa pigo kali kwa mchokozi yeyote,” imeandika: Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu alisisitiza kwamba taifa la Iran litajibu kwa nguvu uchokozi wowote, na wakati huo huo, Iran sio mwanzilishi wa vita, lakini shambulio lolote linaweza kusababisha mzozo wa kikanda. Chombo hicho cha habari pia kimemnukuu Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu akisema kwamba vitisho vya mara kwa mara vya Marekani si vipya na havina athari yoyote kwa irada na azma ya taifa la Iran.

Tovuti ya “Kol Al Arab” pia imeandika katika ripoti yenye kichwa cha maneno kisemacho: “Wamarekani wanapaswa kujua kwamba wakianzisha vita, mara hii vitageuka kuwa vita vya kikanda”: Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu alifafanua kwamba Jamhuri ya Kiislamu haipendi vita, lakini itasimama imara dhidi ya uchokozi wowote.
Kanali ya Televisheni ya Sky News Arabia, ikiakisi hotoba ya Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu imeripoti kwamba Ayatullah Khamenei alionya dhidi ya shambulio lolote la kijeshi la Marekani, akisisitiza kwamba hatua kama hiyo ingesababisha mzozo wa kikanda. Kanali hiyo ya televisheni pia imemnukuu Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu akisema kwamba matukio ya hivi karibuni nchini Iran yanafanana sana na mapinduzi na yalilenga kushambulia vituo nyeti vya serikali.
Tovuti ya “Al-Mamlakah” na gazeti la Lebanon “Al-Diyar” pia vimejikita katika mkondo huo huo na kuripoti kwamba, mashambulizi dhidi ya vituo vya serikali, kambi za kijeshi, benki, na maeneo ya kidini wakati wa matukio ya hivi karibuni yalikuwa ishara ya jaribio la mapinduzi lililoshindwa.
Mashirika ya habari “Sputnik Arabi”, “Kanali ya Televisheni ya al-Akhbariyah, na “Al-Arabi Al-Jadeed” pia yameangazia onyo la Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, yakiripoti kwamba vita vyovyote vya Marekani dhidi ya Iran vitageuka kuwa vita vya kikanda na kwamba taifa la Iran litajibu kwa uthabiti uchokozi wowote.
Kuakisiwa hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika vyombo vya habari vya kimataifa kunadhihirisha jinsi matukio ya Iran yanavyozingatiwa hasa katika siku za hivi karibuni kufuatia vitisho vya mara kwa mara vya Rais Donald Trum wa Marekani dhidi ya taifa hili.
Vitisho vya Trump vimekabiliwa na majibu tofauti kutoka kwa viongozi wa Iran ambayo wanasisitiza kwamba, endapo mara hii kutatokea chokochoko yoyote dhidi ya Iran, basi jibu la taifa hili la Kiislamu litakuwa kali na la kumjutisha adui.