Musoma. Majaji na mahakimu mkoani Mara wametakiwa kutenda haki wakati wa kutimiza majukumu yao, hususan kwenye utoaji wa hukumu wa mashauri mbalimbali, ili kuepuka adhabu ya Mungu pale watakapokwenda kinyume.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Musoma, Fahamu Mtulya, ametoa wito huo leo, Jumatatu Februari 2, 2026, mjini Musoma kwenye maadhimisho ya Siku ya Sheria na kusema majaji na mahakimu wanapaswa kufahamu kuwa kazi yao ni ya kimungu, hivyo waifanye kwa uadilifu mkubwa.
“Tunafanya kazi kwa niaba ya Mungu hapa duniani, asili ya kazi yetu ni ya kiungu. Hivyo, hukumu zetu ziwe za haki. Tutende haki kwa niaba ya Mungu. Tusipotenda haki, kesho tutawajibika kwa Mungu,” amesema.
Jaji Mtulya amesema msingi mkubwa wa maendeleo ya taifa lolote duniani ni haki, hivyo watendaji wa mahakama wanatakiwa kuhakikisha kazi zao zinafanywa kwa kuzingatia haki bila upendeleo wala ubaguzi.
Amesema kunapokuwa na haki, amani pia inakuwepo, hali ambayo inasababisha kuwepo kwa maendeleo ya taifa na watu wake. Kutokana na hali hiyo, mahakama ina wajibu mkubwa katika kuhakikisha nchi inakuwa na maendeleo endelevu kwa kutenda haki.
“Hakuna taifa linalokuwa na maendeleo bila amani, na amani itakuwepo pale penye haki. Kwa hiyo, mahakama ina wajibu mkubwa sana na ni daraja la kufikia maendeleo,” amesema.
Amesema mhimili huo umekuwa ukijitahidi kuboresha huduma zake kwa wananchi, ikiwepo suala la kusogeza huduma karibu ili kuwapunguzia wananchi gharama kubwa walizokuwa wanatumia katika kutafuta huduma za kimahakama.
Ametolea mfano wa Mahakama Kuu Kanda ya Musoma, ambapo kabla ya kuwepo mjini Musoma, wakazi wa Mkoa wa Mara walikuwa wakilazimika kusafiri hadi Mwanza, umbali wa zaidi ya kilomita 220, kutafuta huduma za mahakama Kuu.
Amesema tangu kuanzishwa kwa mahakama hiyo mwaka 2019, jumla ya mashauri 7,709 yamesajiliwa, huku mashauri 7,138 yakitolewa uamuzi, hali ambayo kwa namna moja ama nyingine imewapunguzia gharama na muda wananchi, ambao kama mahakama hiyo isingekuwepo wangelazimika kusafiri hadi Mwanza.
Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Juma Chikoka akizungumza kwenye maadhimisho ya siku ya sheria yaliyofanyika mjini Musoma mkoani Mara. Picha na Beldina Nyakeke
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Juma Chikoka, ameitaka mahakama kuendelea kuwa kimbilio la wananchi kwa kutenda haki, ili kumaliza malalamiko ya wananchi juu ya vitendo vya ukiukwaji wa haki wanavyokutana navyo katika mazingira yao.
Kanali Mtambi amesema watendaji wa mahakama wakifanya shughuli zao kwa weledi na maadili, imani ya wananchi itazidi kujengeka juu ya muhimili huo, hatua ambayo kwa namna moja ama nyingine ina mchango mkubwa kwa ustawi wa jamii nzima.
Amesema imeshuhudiwa kwa kiasi kikubwa namna ambavyo mahakama imefanya mapinduzi makubwa katika utekelezaji wa shughuli zake, ikiwa ni pamoja na kupunguza mlundikano wa kesi mahakamani, jambo ambalo limepunguza pia malalamiko ya wananchi katika ofisi za Serikali.
“Jambo jingine ni namna ambavyo sasa hivi kesi nyingi zinachukua muda mfupi kusikilizwa na kufanyiwa maamuzi mara tu zinapofika mahakamani, tofauti na zamani ambapo kesi zilikuwa zinachukua muda mrefu sana na kusababisha malalamiko mengi sana ya wananchi,” amesema.
Amesema ni vema mahakama ikaendelea na uboreshaji wa shughuli na utendaji wake wa kazi, ili kuendelea kujenga imani ya wananchi kwa kuhakikisha usawa, haki na maendeleo ya taifa.
Akizungumza kwa niaba ya Chama cha Mawakili (TLS), Leonard Magweyega amesema Mahakama ni mhimili wa dola unaotokana na Katiba ya nchi, hivyo ni vema ikatekeleza wajibu na majukumu yake kwa mujibu wa utaratibu.
Amesema mahakama ina mchango mkubwa katika kuamua hali ya utulivu na amani ya nchi pale itakapokiwa, ikifanya majukumu yake kwa haki bila upendeleo wa aina yoyote.
“Taifa likiwa na mfumo mzuri wa haki unaofanya kazi bila dhuluma wala hiyana, basi ustawi wa kiuchumi na kisiasa utaimarika, kwani wananchi wakijua haki itapatikana bila upendeleo, wataelekeza nguvu zao katika shughuli za ujenzi wa taifa,” amesema.
Amesema mahakama inapaswa kuhakikisha panakuwepo uwajibikaji wa mamlaka nyingine nchini bila upendeleo wala ubaguzi, jambo ambalo ni nguzo muhimu kwa ukuaji wa demokrasia nchini kwa maslahi ya nchi na watu wake.