Mtwara. Watumishi wa umma nchini wametakiwa kuzingatia nidhamu, uadilifu, maadili na uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu yao ili kuimarisha utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
Wito huo umetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Xavier Mrope, wakati akizindua Baraza la Sita la Wafanyakazi wa Chuo cha Utumishi wa Umma lililofanyika leo Alhamisi, Juni 11, 2026, mkoani Mtwara.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mrope alisisitiza kuwa uwajibikaji, weledi na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ni msingi muhimu wa kujenga utumishi wa umma wenye tija na unaokidhi matarajio ya wananchi.
Alieleza kuwa watumishi wanapaswa kuzingatia uadilifu, uwajibikaji na ubunifu katika kazi zao, akibainisha kuwa Serikali haitavumilia vitendo vinavyokwenda kinyume na sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma.
Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais – UTUMISHI, Xavier Mrope, akizungumza na wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Chuo cha Utumishi wa Umma.
“Nisisitize sana suala la uadilifu, uwajibikaji na ubunifu viendelee kuwa msingi mkubwa wa utendaji wenu wa kazi. Tunapowajengea uwezo na umahiri watumishi wa umma, tutajisikia vibaya sana tukisikia watumishi wa Chuo cha Utumishi wa Umma wanakumbwa na kasoro za maadili au kulalamikiwa kwa kukosa uwajibikaji,” amesema Mrope.
Aidha, aliwakumbusha watumishi umuhimu wa kuwahudumia wananchi kwa weledi na heshima, akisisitiza matumizi ya lugha nzuri na yenye staha wakati wa kutoa huduma, pamoja na kuwasikiliza na kuwahudumia wateja kwa ufanisi ili kujenga imani na kuridhika kwa wananchi wanaopokea huduma za serikali.
“Lugha za kuwahudumia wateja ziwe nzuri, kwa sababu unapomhudumia vibaya mwananchi, jambo la kwanza linalochafuka ni taswira ya taasisi unayoifanyia kazi, siyo wewe binafsi. Hivyo hakikisheni mnatumia lugha zenye staha mnapowahudumia wananchi,” amesema.
Mrope amesisitiza kuwa watumishi wakizingatia maadili, uadilifu, uwajibikaji na weledi, itasaidia kujenga utumishi wa umma wenye ufanisi na unaozingatia misingi ya kazi za umma.
Katika hatua nyingine, amewataka watumishi wa umma kuboresha matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) kwa kubuni mifumo mipya itakayorahisisha utoaji wa huduma na mafunzo kwa watumishi wa umma pamoja na wananchi kwa ujumla.
Pia amesisitiza umuhimu wa kuimarisha mifumo ya TEHAMA ili iweze kuwasiliana na kufanya kazi kwa pamoja, hatua itakayoongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za umma.
Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo na Mtendaji Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma (TPSC), Ernest Mabonesho, ameeleza umuhimu wa mabaraza ya wafanyakazi katika kuimarisha ushirikiano, uwazi na ushiriki wa watumishi katika maendeleo ya taasisi.
Mkuu wa Chuo na Mtendaji Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma, Ernest Mabonesho, akizungumza katika Baraza la Wafanyakazi la chuo hicho.
Amesema mabaraza hayo yanatoa fursa kwa watumishi kujadili masuala mbalimbali yanayohusu ustawi wa taasisi na mazingira ya kazi, hali inayochangia kuongeza tija na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu.
Aidha, ametaja mafanikio yaliyopatikana katika chuo hicho, akibainisha kuwa katika kipindi cha miaka mitatu mfululizo taasisi hiyo imeendelea kuimarisha utoaji wa mafunzo na huduma kwa watumishi wa umma, sambamba na kuboresha mifumo ya utendaji na usimamizi wa rasilimali watu.
“Napenda kuchukuwa fursa hii, niishukuru Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,kwa kuendelea kukipa chuo fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo ambapo kwa kipindi cha miaka mitatu, imetupa jumla ya Sh8.4 bilioni, kwa hatua tatu” amesema
Nao washiriki wa Baraza hilo, akiwamo Mhadhiri Msaidizi wa Chuo cha Utumishi wa Umma Kampasi ya Dar es Salaam, Suzan Swila, wameeleza kuwa maazimio na mafunzo yanayotolewa kupitia mabaraza ya wafanyakazi yanasaidia kuongeza uwajibikaji, ushirikiano na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku.
Swila amesema mabaraza hayo yanatoa fursa kwa watumishi kujadili changamoto zinazowakabili katika mazingira ya kazi na kupendekeza suluhisho litakalosaidia kuboresha utendaji wa taasisi na utoaji wa huduma kwa wananchi.