
Rais wa Iran Massoud Pezeshkian ameomba kufunguliwa kwa mazungumzo ya nyuklia na Marekani, shirika la habari la FARS limeripoti siku ya Jumatatu, Februari 2. Hii inakuja huku kukiwa na mvutano na Washington, ambayo haijaondoa uwezekano wa matumizi ya nguvu za kijeshi.
Imechapishwa:
Dakika 2 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
“Rais Massoud Pezeshkian ameagiza kufunguliwa kwa mazungumzo na Marekani,” shirika la habari la FARS limeandika, likinukuu chanzo cha serikali. “Iran na Marekani zitafanya majadiliano kuhusu suala la nyuklia,” FARS imeongeza, bila kutaja tarehe. Taarifa hii pia imeripotiwa na gazeti la serikali la Iran na Gazeti la kila siku la mageuzi la Shargh.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi na Mwakilishi wa Marekani Steve Witkoff wanaweza kukutana katika siku zijazo nchini Uturuki au mji mkuu mwingine wa kikanda, anaripoti mwandishi wetu huko Tehran, Siavosh Ghazi. Hakika, Uturuki, Misri, Saudi Arabia, na Qatar zimekuwa zikifanya kazi kama wapatanishi kwa siku kadhaa ili kupunguza mvutano kati ya Tehran na Washington na kuzuia shambulio la kijeshi dhidi ya Iran.
Lakini Tehran inasisitiza kudumisha mpango wake wa kuratubisha uranium kwa matumizi yake ya raia na inakataa kujadili mpango wake wa makombora ya balistiki. Hata hivyo, Marekani inadai kusitishwa kabisa kwa mpango wa nyuklia na kupunguzwa kwa masafa ya makombora ya Iran. Katika hali hizi, mazungumzo hayatakuwa rahisi.
“Uwezekano wa majadiliano”
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alisema mapema kwamba makubaliano yanawezekana na Marekani kuhusu mpango wa nyuklia wa nchi hiyo. Alisema aliona “uwezekano wa majadiliano ikiwa timu ya mazungumzo ya Marekani itafuata kile Rais Trump amesema: makubaliano ya haki na usawa ya kuhakikisha kwamba hakuna silaha za nyuklia” huko Tehran, Abbas Araghchi alisema katika mahojiano yaliyoruhwa siku ya Jumapili na CNN.
Mawasiliano ya kidiplomasia yameongezeka tangu wakati huo. Siku ya Jumatatu asubuhi, Februari 2, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran aliwapigia simu wenzake wa Uturuki, Saudi Arabia, na Misri. “Tunapitia na kukamilisha maelezo ya kila hatua ya mchakato wa kidiplomasia, ambao tunatarajia kuhitimisha katika siku zijazo. Hii inahusu mbinu na mfumo,” ameongeza msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Esmail Baghai katika mkutano na waandishi wa habari uliohudhuriwa na shirika la habari la AFP. Esmail Baghai amekana kupokea makataa kutoka kwa Donald Trump: Iran “haikubali kamwe makataa,” amebainisha.
Rais wa Marekani pia alimepiga hatua kuelekea mazungumzo. “Natumai tutafikia makubaliano,” Donald Trump amewaambia waandishi wa habari. “Ikiwa hatutakubaliana, tutaona kama (Kiongozi Mkuu) yuko sahihi au la,” ameongeza.