Saif al-Islam Gaddafi, mmoja wa watoto wa kiongozi wa zamani wa Libya, Muammar Gaddafi, ambaye kwa muda mrefu alichukuliwa kuwa mrithi wake na alikuwa akitafutwa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kwa uhalifu dhidi ya ubinadamu, ameuawa siku ya Jumanne, Februari 3, vyanzo kadhaa vimethibitisha kwa RFI.

Imechapishwa:

Dakika 2 Wakati wa kusoma

Matangazo ya kibiashara

Kituo cha televisheni cha Libya Al Ahrar kimeripoti kwamba “watu walio karibu” na Saif al-Islam Gaddafi walitangaza kifo chake “bila kufichua mazingira ya kifo hicho.” Mshauri wake na mwakilishi wake katika Kamati ya Kitaifa ya Mazungumzo, Abdullah Othman Abdurrahim, amebainisha kwamba alifariki katika chapisho la Facebook, bila kutoa maelezo zaidi.

“Dkt. Saif al-Islam amefariki dunia,” binamu yake, Hamid Gaddafi, amekiambia kituo cha televisheni cha al-Ahrar kwa simu.

Kikosi cha makomandoo cha watu wanne kinaripotiwa kutekeleza mauaji hayo, kulingana na mshauri wa Saif al-Islam Gaddafi.

Kulingana na vyombo kadhaa vya habari, Saif al-Islam alifariki kusini mwa jiji la Zintan magharibi mwa Libya. Saif al-Islam, 53, alikuwa peke yake nyumbani alipopigwa risasi na watu wanne wenye silaha waliovamia makazi yake baada ya kuzima kamera za usalama. “Walivamia makazi ya Saif al-Islam Gaddafi baada ya kuzima kamera za usalama, kisha wakamwua,” kiliandika kituo cha al-Ahrar cha Libya kwenye mtandao wa kijamii wa X, kikimnukuu Abdullah Othman Abdurrahim kama ilivyoripotiwa na kituo hicho. Wakili wa Saif al-Islam alithibitisha kwa shirka la habari la AFP kwamba “kitengo cha makomandoo cha watu wanne” kilimuua mtoto wa Muammar Gaddafi nyumbani kwake.

Vyanzo vingine vimeishutumu Brigedi ya 444 kwa kutekeleza mauaji hayo. Kikosi hiki, kinachoongozwa na Mahmoud Hamza, kimekana haraka kuhusika kokote katika mauaji hayo. “Tunathibitisha kwamba hakuna vikosi vilivyowekwa Zintan na tunakana kuwepo kwa uamuzi wowote wa kufuatilia Saif al-Islam Gaddafi,” taarifa yao imesema.

“Hatazikwa hadi uchunguzi utakapokamilika”

Picha ya mwili wake ukiwa umelala nyuma ya gari aina ya Toyota inasambaa kwenye mitandao ya kijamii. Mshauri wake wa kisiasa anadai kwamba mwili wake ulipelekwa hospitali ya kibinafsi huko Zintan, na kwamba majaji wanne tayari wamefika jijini kufanya uchunguzi. “Hatazikwa hadi uchunguzi utakapokamilika,” mshauri wake amesema.

Wakili wake, Abdullah Zaydi, amelaani “mauaji ya kutisha ya Saif al-Islam.” Uhalifu mbaya unaoongeza mfululizo wa uhalifu uliofanywa dhidi ya raia wa Libya.

Akionyeshwa kwa muda mrefu kama mrithi mtarajiwa wa baba yake, Saif al-Islam, 53, alikuwa amejijengea taswira kama mtu mwenye msimamo wa wastani na mrekebishaji. Sifa hii ilizima alipoahidi umwagaji damu mwanzoni mwa uasi. Akitafutwa na ICC kwa uhalifu dhidi ya ubinadamu, alikamatwa kusini mwa Libya. Akiwa kizuizini kwa muda mrefu huko Zintan, alihukumiwa kifo mwaka wa 2015 kufuatia kesi kabla ya kupewa msamaha.

Mnamo mwezi Novemba 2021, aliwasilisha ugombea wake wa uchaguzi wa rais, ambao ulipangwa kufanyika mwezi Desemba mwaka huo. Uchaguzi hatimaye haukufanyika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *