Droo ya hatua ya robo fainali ya mashindano ya Klabu Afrika msimu huu imefanyika leo huko Cairo, Misri, ambapo imeviweka mtegoni baadhi ya vigogo huku ikiibua mechi zinazokutanisha timu za nchi moja.

Katika Ligi ya Mabingwa Afrika, RS Berkane ya Morocco imepangwa kukutana na Al Hilal ya Sudan na Esperance ya Tunisia itavaana na Al Ahly ya Misri.

Mechi nyingine za hatua hiyo kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika ni baina ya Mamelodi Sundowns dhidi ya Stade Malien na AS FAR itakabiliana na Pyramids FC.

Timu zitakazokutana katika hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2025/2026. Picha na CAF

Katika hatua ya nusu fainali, mshindi wa mchezo baina ya Esperance na Al Ahly atakutana na timu itakayosonga mbele baina ya Mamelodi Sundowns na Stade Malien.

Nusu fainali nyingine itahusisha mshindi wa mechi baina ya AS FAR na Pyramids FC dhidi ya mshindi kati ya RS Berkane dhidi ya Al Hilal.

Katika Kombe la Shirikisho Afrika, timu mbili za Morocco, Olympic Safi na Wydad Club zimepangwa kukutana katika robo fainali.

Timu zitakazokutana katika hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2025/2026. Picha na CAF

Kutakuwa na mchezo pia baina ya Al Masry ya Misri na CR Belouizda ya Algeria, AS Otoho ya Congo itakabiliana na Zamalek ya Misri huku AS Maniema ya DR Congo ikipangwa kucheza na USM Alger ya Algeria.

Katika nusu fainali, mshindi baina ya Maniema na USM Alger atakabiliana na mshindi baina ya Olympic Safi na Wydad AC.

Nyingine itahusisha mshindi kati ya Al Masry na Belouizdad dhidi ya mshindi baina ya Otoho na Zamalek.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *