
Shirika la kimataifa la Haki za Binadamu la Human Rights Watch limekaribisha vikwazo vilivyotangazwa Machi 2 na Marekani dhidi ya jeshi la Rwanda na maafisa wanne wakuu wa kijeshi kwa kuunga mkono kundi lenye silaha la M23 mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, likizitaka serikali zingine kuchukua hatua kama hizo.
Imechapishwa:
Dakika 2 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Kulingana na shirika hili la haki za binadamu, vikwazo hivi vinawakilisha “juhudi kubwa” ya kutekeleza Makubaliano ya Washington yaliyohitimishwa mwezi Desemba 2025 kati ya marais wa Kongo na Rwanda chini ya upatanishi wa Marekani.
“Vikwazo vya Marekani vinazidi suala la usaidizi wa kijeshi wa Rwanda kwa M23 na vinaonyesha juhudi muhimu ya kutekeleza Makubaliano ya Washington,” amesema Nicole Widdersheim, naibu mkurugenzi wa ofisi ya Human Rights Watch huko Washington. “Marekani inabaini kwamba ushindi wa M23 kuchukuwa udhibiti wa maeneo kadhaa usingewezekana bila ushiriki wa moja kwa moja wa jeshi la Rwanda na kwamba Rwanda lazima ikomeshe usaidizi wake kwa M23 mara moja.”
Ofisi ya Udhibiti wa Mali za Kigeni ya Wizara ya Fedha ya Marekani (OFAC) inasema kwamba jeshi la Rwanda “linaunga mkono kikamilifu, kutoa mafunzo, na kupigana kwa M23,” kundi lenye silaha linaloshutumiwa kwa unyanyasaji mkubwa na kuhusika na mgogoro mkubwa wa watu waliokimbia makazi yao mashariki mwa DRC.
Vikwazo hivyo vinamlenga Jenerali Mubarakh Muganga, Mkuu wa majeshi ya Rwanda; Meja Jenerali Vincent Nyakarundi, Mkuu wa jeshi la nchi kavu; Meja Jenerali Ruki Karusisi, kamanda wa Kitengo cha 5 cha kikosi cha nchi kavu na mkuu wa zamani wa vikosi maalum; na Brigedia Jenerali Stanislas Gashugi, kamanda wa vikosi vya operesheni maalum.
Hatua hizi ni pamoja na kuzuiwa mali zote zinazoshikiliwa nchini Marekani na maafisa hawa au na jeshi la Rwanda na kuwazuia raia wa Marekani kufanya miamala nao. Wizara ya Fedha ya Marekani pia inaonya kwamba taasisi za fedha na wahusika wengine wanaweza kukabiliwa na vikwazo ikiwa watafanya baadhi ya miamala inayowahusisha watu hawa waliotajwa.
Vikwazo hivyo vinakuja baada ya kutekwa kwa mji wa Uvira mnamo Desemba 10, 2025, na vikosi vya M23 na Rwanda, siku chache tu baada ya kusainiwa kwa makubaliano ya amani huko Washington kati ya viongozi wa Kongo na Rwanda.
Kulingana na Human Rights Watch, Umoja wa Mataifa, Marekani, na Umoja wa Ulaya wameorodhesha ukiukwaji mkubwa unaohusishwa na M23, ikiwa ni pamoja na mauaji ya kikatili, unyanyasaji wa kijinsia, watu kuhamishwa kwa lazima, mashambulizi dhidi ya raia, na kuajiri wapiganaji kwa lazima, ikiwa ni pamoja na watoto.
Kulingana na vyanzo vya Umoja wa Mataifa na kijeshi vilivyonukuliwa na shirika hilo, wanajeshi elfu kadhaa wa Rwanda, ikiwa ni pamoja na vikosi maalum, walivuka mpaka na kuingia DRC katika wiki zilizotangulia shambulio dhidi ya mji wa Uvira mnamo mwezi Desemba.
Human Rights Watch inabaini mwitikio wa kimataifa kwa usaidizi wa Rwanda kwa M23 bado hautoshi na inatoa wito kwa serikali zingine, haswa katika Umoja wa Ulaya, Uingereza, na barani Afrika, kupitisha vikwazo dhidi ya maafisa wengine wa M23 na jeshi la Rwanda.
Shirika hilo pia linatetea kuimarisha mifumo ya kufuatilia makubaliano ya amani na kuongeza shinikizo la pande nyingi ili kuwalinda raia na kuhakikisha upatikanaji wa misaada ya kibinadamu mashariki mwa DRC, ambapo mapigano yamesababisha mamia ya maelfu ya watu kuhama makazi yao.