
Sheikh Ibrahim Zakzaky, kiongozi wa Harakati ya Kiislamu nchini Nigeria ametuma salamu za rambi rambi kufuatia kuuawa shahidi Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei.
Kwenye ujumbe huo, Sheikh Zakzaky ameelezea hasara kubwa na maumivu yake kufuatia tukio hilo chungu huku akitangaza kufungamana na familia ya Shahidi Imam Khamenei, wannazioni wa Kiislamu na wananchi wa Iran, Ummah wa Kiislamu, na wanaodhulumiwa duniani.
Amesema: “Mauaji haya ni kinyume cha ubinadamu na ya kiwoga ni hujuma ya wazi dhidi ya binadamu wote.”
Sheikh Zakzaky alisisitiza kuwa, hatua hii ya kuua haitadhoofisha azma ya watu katika kukabiliana na ugaidi, udhalimu na ukosefu wa uadilifu.
Sheikh Zakzaky aliwahi kutembelea Iran na kukutana na Imam Khamenei.
Marekani na Israel zilianzisha hujuma za kigaidi dhidi ya Iran Jumamosi tarehe 28 Februari na kumuua Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, wakuu wengi wa kijeshi, na raia mamia wakiwemo watoto wengi.
Katika kujibu uchokozi huo, Iran imetangaza kulipiza kisasi kwa mashambulizi ya kijeshi yajulikanayo kama ‘Ahadi ya Kweli 4’ ambapo imetumia makombora na ndege zisizo na rubani kulenga ngome za kijeshi, kiuchumi na kijasusi za utawala haramu wa Israel na vituo vya kijeshi na kijasusi vya Marekani vilivyo katika ardhi za nchi za eneo.